Pande hasimu Sudan zafikia makubaliano mapya ya usitishaji vita ya saa 72
Pande mbili zinazopigana nchini Sudan, jeshi la taifa SAF na kikosi cha uusaidizi wa haraka (RSF), zimekubaliana kusitisha mapigano kwa saa 72 kuanzia Jumapili ya leo.
"Ufalme wa Saudi Arabia na Marekani zimetangaza kufikiwa makubaliano ya wawakilishi wa Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) kwa ajili ya kusitisha mapigano kwa muda wa saa 72 kuanzia Jumapili. Hayo yametangazwa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Saudi Arabia.
Hii si mara ya kwanza pande hizi mbili kutangaza makubaliano ya kusitisha mapigano kwa kipndi fulani na baadaye yanavunjika na pande hasimu Sudan kurejea kwenye meza ya mazungumzo.
Makubaliano kadhaa ya kusitisha vita hapo nyuma yamekuwa yakivunjika. Mnamo mwisho wa mwezi Mei, Marekani iliwawekea vikwazo majenerali wanaohasimiana wa pande hizo mbili, ikiwashutumu kwa kile ilichokiita umwagaji damu wa kutisha.
Wakati huo Wizara ya Afya ya Sudan imetangaza kuwa, idadi ya watu waliouawa katika mapigano yanayoendelea kushuhudiwa nchini humo ni zaidi ya elfu tatu.
Haitham Muhammed İbrahim, Waziri wa Afya wa Sudan ameongeza kuwa, mapigano hayo yaliyoanza tangu Aprili 15 yamesababisha pia watu elfu sita kujeruhiwa.
Idara ya Afya jijini Khartoum iliripoti jana Jumamosi kwamba, watu 17 wakiwemo wanawake na watoto wadogo wameuawa katika shambulizi la anga katika eneo la Yarmouk, kusini mwa mji mkuu huo wa Sudan, mbali na nyumba 25 kuharibiwa.
Vita vya Sudan viliingia mwezi wa tatu Alkhamisi iliyopita, huku mashirika mbalimbali ya misaada ya kibinadamu ya kieneo na kimataifa yakitahadharisha kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu nchini humo na kutoa mwito wa kusitishwa vita hivyo.