Al Azhar yalaani hujuma ya Wazayuni na kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu
Taasisi ya al Azhar nchini Misri imelaani vikali kitendo cha walowezi wa Kiyahudi cha kuchoma moto na kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu.
Al-Azhar ya Misri imetoa taarifa hiyo leo Jumapili ikilaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu cha walowezi wa Kizayuni wakati wa mashambulizi dhidi ya misikiti ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kutangaza kuwa, umefika wakati wa kuchukua msimamo mmoja na madhubuti wa Kiarabu na Kiislamu dhidi ya utawala ghasibu wa Israel ambao umefanya jinai mbaya zaidi dhidi ya Wapalestina. Taarifa hiyo imesisitiza kuwa hatua za haraka na madhubuti lazima zichukuliwe ili kuanzisha taifa huru la Palestina mji mkuu wake ukiwa Quds Tukufu.
Awali Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ilitoa taarifa ikilaani kitendo cha walowezi wa Kizayuni huko Nablus cha kuvamia misikiti na kuchoma moto nakala za Qur'ani Tukufu na kusisitiza kuwa: Hii ni jinai ya kinyama inayochochea vita vya kidini vya taasisi za Kizayuni dhidi ya watu wa Palestina.
Wakati huo huo, harakati ya Jihad Iislami ya Palestina sambamba na kulaani kitendo cha Wazayuni kuchoma moto Qur'ani Tukufu huko Nablus, imetangaza kuwa: "Kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu ni katika mfululizo wa mashambulizi yanayofanywa na Israel dhidi ya watu wa Palestina na kunachochea zaidi mapambano ya ukombozi ya Wapalestina. Jihad Islami imeongeza kuwa: Kitendo hiki hatari kinaonyesha hamu ya adui mwenye kichaa ya kuwasha moto wa vita vya kidini.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia amelaani vikali kitendo cha walowezi wa Kizayuni cha kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu wakati wa mashambulizi ya askari wa Israel dhidi ya misikiti katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Walowezi wa Kizayuni Alkhamisi usiku walivamia Msikiti wa al-Ribat katika kitongoji cha Urif kusini mwa mji wa Nablus, na kuchoma moto nakala za Qur'ani Tukufu. Video ya kamera ya CCTV imeonyesha Wazayuni hao waliokuwa wamefunika nyuso zao wakichana na kuchoma moto nakala za Qur'ani Tukufu ndani ya msikiti huo.
Walowezi hao wa Kizayuni hawakuishia hapo, bali walienda mbali zaidi na kuingiza mbwa ndani ya msikiti huo. Vitendo hivyo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu vimeumiza hisia za Waislamu kote dunia.