Ulimwengu wa Michezo, Jul 29
(last modified Mon, 29 Jul 2024 07:19:45 GMT )
Jul 29, 2024 07:19 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Jul 29

Hujambo msikilizaji mpenzi, natumai u mzima wa afya. Kipindi chetu cha leo ni makhsusi kwa ajili ya kuangazia tathmini na dondoo za Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024. Mashindano ya mara hii, yanatumika si tu kama jukwaa la kuitetea Palestina, bali pia ni uwanja wa kulaani na kukosoa jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel na waitifaki wake Wamagharibi, dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Huku Michezo ya Olimpiki ya Paris ya mwaka huu wa 2024 ikiendelea nchini Ufaransa, upinzani wa kimataifa dhidi ya ushiriki wa timu ya utawala wa Kizayuni katika michezo hiyo nao umeongezeka. Michezo ya Olimpiki ya msimu huu wa joto kali huko Paris, mji mkuu wa Ufaransa ilianzia Ijumaa iliyopita ya Julai 26 na itaendelea hadi Agosti 11. Kabla ya kuangazia upinzani dhidi ya Israel kwenye mashindano hayo, tugusie ufunguzi wa michezo hiyo ambao wenyewe umekabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii na hata viongozi wa kidini. Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Ufaransa limekosoa kitendo cha kuvunjiwa heshima nembo na matukufu ya Kikristo kwenye ufunguzi huo, na kutumika kama jukwaa la kushajiisha ufuska, ushoga, ushirikina, na kufuru.

Viongozi wa dini ya Kikristo wamewakosoa waandaaji wa hafla ya ufunguzi wa mashindano hayo, hasa kutokana na onyesho la "Drag Queens" la mwanamume aliyevaa mavazi ya kike na kujikwatua na taswira ya mchoro wa “Karamu ya Mwisho,” (Last Supper) ambayo baadhi wanasema inaonyesha picha ya Nabii Isa AS, na wanafunzi wake.

Baadhi ya vipengele vya maonyesho ya ufunguzi huo vimekosolewa vikali, vikitajwa kuwa ni kampeni ya imani za kishetani na kueneza ushoga, haswa kipengee cha tamthilia ya picha ya "Karamu ya Mwisho" ya Leonardo da Vinci, kupitia wahusika waliobadilisha jinsia (Drag Queens), ambayo wakosoaji wanasema kuwa ni tusi la kimakusudi kwa Ukristo na dini za Mwenyezi Mungu. Katika hafla hiyo ya Michezo ya Olimpiki Paris 2024, nafasi ya "Kristo" katika uchoraji wa Karamu ya Mwisho, aliwekwa mtu aliyekuwa uchi, ambaye wakosoaji wanasema kwamba aliwakilisha Dionysus, mungu wa divai ambaye pia alijulikana kwa desturi zake za kipagani na zisizo na maadili. Maaskofu wa Ufaransa wamewashukuru wafuasi wa dini nyingine kwa kuonyesha mshikamano wao na Wakristo katika kukabiliana na upumbavu huo.

********************

Katika hatua nyingine, kampeni ya "Hakuna Olimpiki, Hakuna Mauaji" kwa ajili ya kutaka kuondolewa Israel katika mashindano hayo ya kimataifa ingali inaendelea. Maandamano dhidi ya Wazayuni yameongezeka duniani kote, ikiwa ni pamoja na miji mbalimbali ya Ufaransa. Wanariadha wa utawala huo katili wanashiriki katika michezo ya Olimpiki ya Paris licha ya mauaji ya halaiki na ya wazi yanayofanywa na utawala wao katika Ukanda wa Gaza. Kabla ya kuanza mashindano hayo ya dunia, Nkosi Zwelivelile Mandela, Mjukuu wa Nelson Mandela, shujaa na kiongozi wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini alitoa mwito wa kuwepo harakati za kimataifa za kuharakisha suala la ukombozi wa Palestina; sambamba na kupigwa marufuku utawala haramu wa Israel kushiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024.

Mandla Mandela

"Mandla" Mandela amesema Wapalestina zaidi ya 400 waliopaswa kushiriki mashindano hayo ya kimataifa huko Ufaransa wameuawa pamoja na wakufunzi wao kwa mabomu ya Wazayuni.

*****************

Wakati huo huo, Kamati ya Olimpiki ya Palestina hivi karibuni ilimwandikia barua Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, ikitaka utawala wa Kizayuni uondolewe katika Michezo ya Olimpiki ya Paris. Katika barua hiyo kwa Rais wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki, Thomas Bach, Kamati ya Olimpiki ya Palestina imeashiria maoni ya hivi karibuni ya Mahakama ya Juu ya Umoja wa Mataifa kuhusu kutokuwa na uhalali ukaliaji kwa mabavu ardhi ya Palestina unaofanywa na Israel na kutaka utawala huo wa Kizayuni uondolewe kwenye Michezo ya Olimpiki ya Paris.

******************

Huku hayo yakiarifiwa, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa, tuhuma zilizotolewa na waziri wa utawala katili wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu kuhusiana na Michezo ya Olimpiki ya Paris ni jaribio lililofeli la kupotosha fikra za walimwengu kuhusiana na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huu huko Gaza. Ni baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Israel Kats, kudai katika barua iliyochapishwa na Reuters siku ya Alkhamisi kwamba, utawala huo una tathmini ya uwezekano wa tishio kutoka kwa wawakilishi wa Iran na eti mashirika mengine ya kigaidi ambayo amedai yanapanga mashambulizi dhidi ya wawakilishi na watalii wa Israel wakati wa Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024! 

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran

Hata hivyo waziri huo wa utawala katili wa Israel hakutoa ushahidi wowote kuhusu madai hayo. Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran, Nasser Kan'ani, amelaani tuhuma hizo dhidi ya Iran na kuongeza kuwa, tuhuma za waziri wa utawala wa mauaji ya watoto wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024 ni jaribio lililofeli la kutaka kugeuza maoni ya umma ili walimwengu wasitilie maanani mauaji ya kimbari yanayoendelea katika Ukanda wa Gaza, na kutaka kukwepa hasira na chuki ya kimataifa kwa vita na jinai za utawala huo dhidi ya watu madhulumu wa Palestina.

Maelfu ya watu wamekuwa wakiandamana mjini Paris wakitaka Israel ipigwe marufuku kushiriki Michezo ya Olimpiki ya mwaka huu kutokana na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo katika eneo la Ukanda wa gaza huko Palestina.

Kulaaniwa Israel katika Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024

Na kwa kutamatisha, Ufaransa imekosolewa vikali kwa uamuzi wake wa kuwazuia wanariadha wa nchi hiyo wanaovaa vazi la staha la hijabu kushiriki ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki iliyoanza mjini Paris Ijumaa.

....................MWISHO.............