Ulimwengu wa Michezo Januari 13, 2025
(last modified Sat, 18 Jan 2025 07:18:56 GMT )
Jan 18, 2025 07:18 UTC

Karibuni wapenzi wa spoti katika dakika hizi chache za kutupia jicho habari mbalimbali za Ulimwengu wa Michezo. Huenda leo kipindi chetu kikaangalia engo tofauti na tulivyoizoea ya michezo. Lakini pia tutavinjari kwenye viwanja mbalimbali vya spoti kama pale nyasi zilipowaka moto kwenye uwanja wa Gombani, mkoa wa Kusini Pemba katika mashindano ya Mapinduzi Cup, lakini zaidi tutajikita zaidi kwenye engo mpya kidogo. Mtayarishaji na msimulizi wako wiki hii ni mimi Ahmed Rashid.

Michezo na Muqawama; mwanasoka wa Palestina, Abu Tima

Tunaanza na Muqawama katika michezo na kadhia nzima ya Palestina. Hatua ya Israel ya kuwaua kigaidi wanamichezo wa Palestina katika jinai zake za Ghaza, zimeendelea kupingwa kwa hisia kali na wanamichezo wa mataifa mengine duniani. Kwa kujikumbusha tu ni kwamba, Mwezi Oktoba 2024, Israel iliendelea kufanya jinai zake kwa kumuua mwanasoka wa Kipalestina pamoja na familia yake huko Ghaza. Imad Abu Tima aliingiia kwenye orodha ya wanamichezo wa Palestina aliyeuliwa kigaidi na kikatili na Israel. Lakini cha kushangaza ni kwamba hadi leo hii, FIFA imekataa kuutimua utawala wa Kizayuni kwenye mashindano yake. Mwanakabumbu wa Kipalestina, Abu Tima na familia yake waliuawa shahidi katika shambulio la kigaidi la anga lililofanywa na Israel Jumanne ya tarehe 15 Oktoba 2024 mashariki mwa kambi ya wakimbizi ya Khan Yunis, kusini mwa Ukanda wa Ghaza. Mwanasoka huyo nguli aliuawa shahidi akiwa na umri wa miaka 21 tu. Abu Tima ambaye alikuwa akikipiga kwenye timu ya Ittihad Khan Yunis, aliwahi kuiwakilisha pia timu ya taifa ya Palestina ya wachezaji wenye umri wa chini ya miaka 20 mwaka 2021. Lakini ‘kaanlam yakun,” kama vile hakuna chochote kilichotokea, Shirikisho la Soka Duniani FIFA halikuipa adhabu yoyote Israel. Ukiangalia hili na ukitupia jicho vikwazo vikali vya michezo ilivyowekewa Russia na mashirika hayo hayo yanayojifanya ni ya kimataifa, utaona ni kiasi gani siasa za Kizayuni za kinafiki na nyuso mbili zinavyotawala katika kila kona ya dunia hii.

**********

UZEMBE WA FIFA HAUJAZUIA KUUNGWA MKONO PALESTINA

Lakini uzembe huo wa FIFA haujawazuia wanamichezo mbalimbali duniani kuendelea kuiunga mkono kadhia ya Palestina. Wiki hii kulienea mkanda wa video unaoonesha jinsi wanamichezo wa Marekani wanavyoendelea kuwa bega kwa bega na kadhia ya Palestina na kuunga mkono wananchi madhlumu wa Ghaza. Mkanda huo wa video ulisema: Hivi ndivyo wanamichezo wa Marekani wanavyosimama imara kuitetea Palestina licha ya kukashifiwa na kuandamwa na vitisho vya kila namna. Katika video hiyo iliyosambaa sana mitandaoni, mchezaji wa Marekani wa mpira wa vikapu na nyota wa NBA All-Star mara nane, Dwight Howard, anazungumzia upinzani aliokumbana nao baada ya kuandika kwenye mtandao wa kijamii wa X maneno yasemayo: "Palestina Huru" au “Komboa Palestina.” Ikumbukwe kuwa, hadi hivi sasa zaidi ya Wapalestina 46,500 wameshauliwa kikatili na Israel, lakini imekuwa nongwa angalau kuandika maneno mawili tu ya “Komboa Palestina.” Katika mahojiano aliyofanyiwa kwenye The GAUDs Show, NBA All-Star mara nane (2007-2014) alisema, hatua yake ya kuiunga mkono Palestina imekaribia kumtumbukiza kwenye hatari ya kupoteza nafasi yake katika ligi ya kulipwa ya mpira wa vikapu nchini Marekani. Alisema: Katika kipindi cha chini ya dakika kumi baada ya kutweet, nilipokea simu za dharura kutoka kwa kamishna wa NBA, mawakala wangu, wawakilishi kutoka taasisi yangu na hata nilipokea simu kutoka Texas wakinitaka kufuta tweet hiyo.” Howard si mwanamichezo pekee aliyeonesha msimamo imara wa kuwaunga mkono Wapalestina licha ya mashinikizo na vitisho vya kila namna dhidi yao. Wanamichezo kama Azeez Al-Shaair, Kyire Irving, Jaylen Brown, Natasha Cloud, Kierstan Bell… orodha ni ndefu… ni miongoni mwa wanamichezo ambao wameonesha waziwazi uungaji mkono wao kwa wananchi madhlumu wa Palestina licha ya kujeliwa, kutishwa na kuvunjiwa heshima.

**********

MOTO WA CALIFORNIA KUIPOKA MAREKANI UENYEJI WA OLIMPIKI?

Hebu tuangalie engo nyingine. Moto wa California kuipoka Marekani uenyeji wa michuano ya Olimpiki? Ni moja ya vichwa vya habari za michezo zilizoakisiwa wiki hii. Habari hiyo imesema: Moto unaoendelea kuiteketeza Los Angeles hivi sasa katika jimbo la California la Marekani hauhatarishi tu maisha ya watu, wanyama, miti na nyumba, bali pia mustakabali wa Michezo ya Olimpiki ya Los Angeles 2028 nao uko hatarini. Moto huo mkali sana ambao umeshateketeza zaidi ya ekari 35,000 na kuharibu vitongoji na maeneo muhimu huko Los Angeles, unahatarisha pia maeneo ya michezo ambayo yamepangwa kutumika kwa ajili ya Michuano ya Olimpiki ya 2028. Habari hiyo imesema: Je, Japan kuwa mwenyeji wa mashindano hayo badala ya Marekani?

*********

MICHEZO IRAN, PERSPOLIS YATAMBA

Kwa hapa Iran, wiki hii timu machachari ya Persepolis imetoa tamko ikitamba kwamba: Bado ina matumaini ya kutwaa ubingwa licha ya kwamba haina kocha wa kigeni. Klabu ya Persepolis ilitoa tamko hilo katika mkesha wa mechi ya Kombe la Super Cup la Iran, ikiandika: "Bado tuna imani ya kutwaa ubingwa katika mazingira mapya na ya kusisimua, na hata bila ya kuwa na kocha wa kigeni.” Habari nyingine inasema: Mohammad Reza Safdarian amesema baada ya kushinda taji la ubingwa kwenye Kombe la Dunia la Kupanda Barafu huko Korea Kusini kwamba: "Niliweza kushinda medali 4 za dhahabu na 4 za fedha ndani ya siku 2." Nimefarijika sana kuona jinsi wananchi wa Iran walivyofurahia medali hizo.

*************

MAPINDUZI CUP! MABINGWA NI ZANZIBAR HEROES

Zanzibar Heroes Hatimaye amekuwa mabingwa wa Mapinduzi Cup. Michuano Sherehe za Mapinduzi Zanzibar kwa mwaka huu zimefanyika kwenye uwanja wa Michezo wa Gombani, katika viunga vya jiji la Chake, mkoa wa kusini Pemba. Mashindano hayo yalikuwa na vimbwanga vingi, lakini hatimaye Zanzibar na Burkina Faso ndio waliotinga fainali. Siku nne nyuma gazeti la Taifa Leo la Kenya liliandika: Harambee Stars inahitaji sare tu kuweza kutinga fainali za Mapinduzi Cup huko Zanzibar, lakini walizamishwa kwenye mkondo wa Nungwi kwa kuchabangwa bao moja bila jibu na miamba ya Zanzibar na kuzimwa ndoto yao ya kupiga makasia na kurejea Kenya wakiwa wamebeba juu kombe hilo. Wababe wengine waliotinga fainali kwenye michuano ya Mapinduzi Cup walikuwa ni vijana wa afande Ibrahim Traoré yaani Burkina Faso. Tanzania Bara yaani Kilimanjaro Stars imeboronga vibaya sana kwenye michuano hiyo. Haikuamulia hata pointi moja. Jumatatu, Januari 13, 2025 ndiyo siku nyasi za Uwanja wa Gombani zilipoteketea chini ya daluga za miamba miwili, Zanzibar na Burkina Faso. Zanzibar waliichabanga Burkina Faso mabao mawili kwa moja na kutwaa kombe hilo.