Filamu, Dini na Mwanadamu wa Sasa-2
Hii ni sehemu ya pili na ya mwisho ya makala ya Dini Katika Filamu.
Katika kipindi cha wiki iliyopita tulisema kuwa licha ya kwamba sehemu kubwa ya filamu duniani imeshambuliwa na masuala ya utumiaji mabavu, vitendo vya kikatili na wakati mwingi filamu za ngono na vitendo vya kuchochea matanio ya kinafsi, lakini kumefanyika juhudi kubwa katika sanaa hiyo za kutengeneza filamu zenye mwelekeo wa masuala ya kiroho na kidini katika miaka ya hivi karibuni.
Katika kipindi kilichopita tuliashiria baadhi ya watengenezaji wa filamu za aina hiyo huko Ulaya na Marekani. Kipindi chetu cha leo kitaelekea Mashariki mwa dunia na kuangalia mtazamo wa watengeneza filamu wa eneo hilo kuhusu masuala ya kiroho na kidini.
Pale unapozungumziwa utamaduni wa Mashariki mwa dunia watu wengi wa Magharibi huwa na taswira ya picha mchanganyiko wa masuala ya kustaajabisha na yaliyojaa siri. Twabaan, mambo kama haya hayana uhakika wowote na huenda yametokana na historia ya utamaduni wa kale wa eneo la Mashariki mwa dunia ambako falsafa, sanaa na elimu vilifungamanishwa na masuala ya teolojia. Kwa msingi huo kumekuwa kukizungumziwa elimu ya irfan (mystery) na falsafa ya Ishraq (Illumination) ambavyo kimsingi vinafungamana na utamaduni wa Mashariki mwa dunia.
Katika medani ya filamu, Wamagharibi hususan watengeneza filamu mashuhuri wa eneo hilo la dunia kama vile Bernardo Bartolucci, Wim Wenders na Alan Rene, wametilia maanani mno utamaduni wa kale wa Mashariki mwa dunia. Wakati huo huo tunapaswa kukiri kwamba, filamu zilizotengenezwa na watengenezaji filamu hao kuhusu utamaduni wa kidini wa kiroho wa Mashariki hazikuakisi kikamilifu masuala yote ya kidini na kiroho ya watu wa eneo hilo. Nyingi kati ya filamu hizo zimezungumzia masuala ya kijuujuu na kidhahiri tu ya dini na desturi za kiirfani za watu wa Mashariki. Nukta ya kutiliwa maanani hapa ni kwamba, jambo linaloonekana zaidi katika filamu hizo ni mkabala wa wazi wa itikadi za kimaada za Magharibi na irfan na masuala ya kiroho ya watu wa Mashariki mwa dunia.
Baada ya utangulizi huo mfupi hebu sasa tuangalie ni maudhui gani za kidini zilizozungumziwa katika filamu za Mashariki.
Tunapochunguza kwa makini tunaona kwamba, kwa ujumla filamu za Mashariki ikiwa ni pamoja na Iran, China, Japan na India, zimegusia masuala na maudhui iliyopewa kipaumbele na watengeza filamu wa eneo hilo kwa ujumla. Masuala hayo yanajumuisha kadhia kama vile kutukuza na kuheshimu familia, ada na desturi za kidini, utambulisho asilia wa watu wa eneo hilo na kadhalika.
Utamaduni wa Mashariki huitambua familia kuwa ni msingi mtukufu wa jamii, kwa maana kwamba, kulinda familia ni muhimu mno katika njia ya kulinda na kuheshimu matukufu ya akhlaki na maadili mema ya jamii. Filamu za Mashariki zimeupa kipaumbele mfungamano wa kifamilia na kuitambua ndoa kuwa ni jambo takatifu. Filamu za eneo hilo zinaitambua familia kuwa ni jamii ndogo inayoakisi sifa na sura halisi ya eneo au jamii ya watu fulani. Filamu hizo zinazotupia jicho masuala ya familia zinaweza kuorodheshwa katika safu ya filamu za kidini na kiroho za Mashariki mwa dunia ambako dini huwa na taathira kubwa katika maisha ya mtu binafsi na jamii kwa ujumla.
Watengenezaji filamu wa Mashariki aidha wamezungumzia maudhui za kihistoria katika medani ya dini na masuala ya kiroho. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, historia ni njia na dirisha la kuvumbua utambulisho wa kitamaduni wa mataifa mbalimbali. Filamu kama vile "The Chess Players" (Shatranj ke Khilari) iliyotengenezwa na Satyajit Rai au Kagemusha (The Shadow Warrior) ya Akira Kurosawa ni mfano wa filamu ambazo shakhsia wake wako katika mikakati ya kutambua utambulisho na sili yao. Filamu hizo zinazungumzia suala la kurejea kwenye asili na mizizi kwa msingi wa falsafa ya Mashariki na kuheshimu waliotangulia kuwa ni sera makhsusi ya mwanadamu anayefuata mafundisho ya dini. Nukta ya kuzingatiwa ni kuwa, athari za sanaa zilizosalia tangu zama za kale kama vile michoro, mashairi, tamthilia, ngonjera na kadhalika vinatazamwa katika filamu za Mashariki kuwa ni njia ya kurejea kwenye asili na chemchemi ya masuala ya kiroho na kimaanawi. Mashairi ya Upanishad ya India, Haiku huko Japan na turathi kubwa ya mashairi ya maurafaa wa Kiirani yanaorodheshwa katika mlolongo huo. Aidha tamthilia kama ile ya "Tabuki" huko Japan, michezo na dansi ya "Kathakali" nchini India na "Taazia" inayofanyika hapa nchini Iran ni miongoni mwa matunda ya sanaa ya Mashariki inayofungamana na dini ambayo imetumika pia katika filamu katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa mujibu wa mtazamo wa watengeneza filamu wengi wa Mashariki, mwanadamu hakuachwa hivi hivi juu ya uso wa dunia. Kwa mujibu wa filamu za Mashariki, hakuna makabiliano yoyote baina ya idara na matwaka ya Mwenyezi Mungu kwa upande mmoja na takdiri ya mwanadamu kwa upande wa pili, kama ilivyo katika falsafa ya Magharibi. Filamu za Mashariki mwa dunia zinakuona kurejea mwanadamu kwenye asili na mwanzo wake kuwa ni suala muhimu na kuyafungamanisha matendo yake yote na Mola Muumba ambaye ndiye chanzo cha dunia na vyote vilivyomo.
Filamu za Iran ni mfano mzuri wa kurejea kwenye dini na masuala ya kiroho na kuzungumziwa mafundisho ya dini katika sinema za Mashariki mwa dunia katika miaka ya hivi karibuni. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, sekta ya filamu ilikumbwa na mabadiliko makubwa. Tokea wakati huo itikadi na mafundisho ya kidini yalichukua nafasi muhimu katika tasnia ya filamu. Filamu zilizotengenezwa hapa nchini baada ya kipindi hicho zilileta mazingira mapya yaliyotofautisha filamu za sasa na zile za kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu na hata maeneo mengine duniani. Dini katika filamu za Iran na katika mtazano wa Kiislamu wa watengeneza filamu wa Kiirani haitazamwi kama njia na desturi makhsusi za mtu binafsi na jamii pekee, bali ni jambo linalohusu maisha yote ya mwanadamu. Katika mtazamo huo, dini inagusa na kuingia katika mambo yote ya maisha, na ina ufumbuzi na jibu la kila kitu. Yumkini baadhi ya filamu zisijumuishe baadhi ya ada za kidhahiri za kidini, lakini bila shaka, roho na batini ya filamu hizo imejengeka juu ya msingi wa itikadi za kidini. Kwa msingi huo, filamu nyingi zinazotengenezwa na watengeneza filamu wa Kiirani zinaweza kuorodheshwa katika safu ya filamu za kidini. Filamu hizo zimejaa masuala mengi ya kiroho na kiteolojia yanayohitajika katika maisha ya kila siku ya mwanadamu. Mfano mzuri wa filamu hizo ni kama ile ya "Mlinzi", "Mhamiaji", "Shamba la Baba", "Ardhi ya Jua", "Mbali Sana, Karibu Sana" na kadhalika ambazo zimekuwa na mafanikio makubwa si kwa watazamaji wa ndani tu bali zimewavutia pia watu wengi katika pembe mbalimbali za dunia.