Rais Rouhani akutana na Papa Francis Vatican
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i10-rais_rouhani_akutana_na_papa_francis_vatican
Rais Hassan Rohani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mapema leo amekutana na kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis kwenye makao makuu ya kanisa hilo huko Vatican.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 26, 2016 11:31 UTC
  • Rais Rouhani akutana na Papa Francis Vatican

Rais Hassan Rohani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mapema leo amekutana na kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis kwenye makao makuu ya kanisa hilo huko Vatican.

Rais wa Iran na Papa Francis wamesisitiza umuhimu wa kushadidishwa vita dhidi ya ugaidi na misimamo mikali. Papa amezungumzia matatizo yanayolikabili eneo la Mashariki ya Kati na kusisitiza kuwa, Iran ni nchi yenye nafasi ya kipekee katika eneo hilo na kwa mantiki hiyo inapaswa kushirikishwa katika michakato yote ya kutatua matatizo ya kieneo. Kabla ya kuonana na Papa Francis huko Vatican, Rais Rouhani alikutana na Waziri Mkuu Matteo Renzi na Rais Sergio Mattarella mjini Rome, Italia. Akizungumza mjini Rome katika siku yake ya pili ya ziara rasmi nchini Italia, Rais Rouhani amesema njia bora zaidi ya kuondoa tatizo la misimamo mikali katika eneo la Mashariki ya Kati ni kuhakikisha uchumi wa eneo unakuwa kwa kiwango cha kuridhisha. Amesema ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana na hali mbaya ya kiuchumi katika nchi za Mashariki ya Kati vimesababisha vijana kurubuniwa kwa wepesi na kukubali kujiunga na makundi yenye misimamo ya kufurutu ada. Rais wa Iran amewakaribisha wawekezaji wa Italia kuja kuwekeza hapa nchini akisema taifa hili linatoa fursa mpya kwa wawekezaji na wajasiriamali baada ya vikwazo vya kiuchumi dhidi ya nchi hii kuondolewa wiki mbili zilizopita. Tayari Iran imesaini makubaliano 14 ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na Italia. Dkt. Rouhani amedokeza kuwa, Waziri Mkuu wa Italia, Mateo Renzi huenda akaitembelea Iran katika kipindi cha miezi kadhaa ijayo ili kuimarisha zaidi uhusiano wa pande mbili.

Rais Hassan Rouhani anatarajiwa kuelekea Ufaransa baada ya kumaliza safari yake nchini Italia.