Mahakama ya Iran kuwashtaki magaidi 100 wa MKO
Mahakama kuu ya jinai ya Iran inatazamiwa kuwapandisha kizimbani wanachama zaidi ya 100 wa kundi la kigaidi la Munafikin (MKO) ambalo limefanya mauaji ya makumi ya maelfu ya wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu.
Shirika la habari la Mizan lenye mfungamano na Idara ya Mahakama ya Iran limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, Tawi Nambari 1 la Mahakama ya Jinai ya Tehran limetangaza kuwa wanachama 104 wa MKO akiwemo kinara wao, Maryam Rajavi wanapaswa kuarifisha mawakili wao watakaowatetea mbele ya mahakama hiyo.
Taarifa ya korti hiyo imesema iwapo mawakili hao hawataarifishwa, basi chombo hicho cha sheria kitalazimika kutoa uamuzi unaoendana na sheria, dhidi ya magaidi hao wa kundi la kigaidi la MKO, wenye historia ya kufanya jinai kubwa.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kuwa, nchi za Ulaya na Marekani ni washirika wa kundi la kigaidi la Munafikin (MKO) katika mauaji ya watu wa Iran.
Aidha Tehran imekuwa ikizikosoa nchi za Magharibi kwa kulipatia hifadhi na himaya kundi hilo la magaidi, ambapo fedha za walipa kodi wa Ulaya na Marekani ndizo zinazokidhi mahitaji ya kundi hilo katili.
Wamagharibi wanaliunga mkono waziwazi kundi la kigaidi la Muunafiqin ambalo faili lake la mauaji ya raia zaidi ya 17,000 wa Iran wasio na hatia liko wazi na bayana.