Ubalozi wa Iran Uhispania: Kuendelea kudhalilishwa Qur'ani Tukufu ni jinai ya kiutamaduni
Ubalozi wa Iran nchini Uhispania umelaani kitendo cha Qur'ani Tukufu kuendelea kuvunjiwa heshima na kukitaja kuwa jinai ya kiutamaduni ambapo pia umekosoa misimamo dhaifu ya Umoja wa Ulaya kuhusiana na suala hilo.
Ubalozi wa Iran nchini Uhispania umetoa taarifa kuhusu kitendo cha kuendelea udhalilishaji wa matukufu ya Kiislamu katika baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya ambapo umetumia maneno makali kulaani kitendo hicho na kusema umefikisha malalamiko yake mbele ya wakuu wa hivi sasa wa Umoja wa Ulaya, na kuutaka umoja huo utoe jibu kali kulaani kitendo hicho.
Salwan Momika raia wa Uwsidi akiwa na raia mwingine wa nchi hiyo wameichoma moto tena nakala ya Quran Tukufu, mara hii mbele ya majengo ya Bunge la Uswidi. Mapema Alhamisi, Julai 20 na ikiwa ni mara ya pili katika kipindi cha wiki chache, Salwan Momika alitekeleza kitendo hicho kiovu cha kudhalilisha Quran Tukufu kwa msaada na ulinzi wa polisi wa Uswidi; kitendo cha matusi ambacho kimewakasirisha sana Waislamu na nchi za Kiislamu.

Baada ya hapo, wanachama wa kundi la itikadi kali na chuki dhidi ya Uislamu la mrengo wa kulia la Denmark linaloitwa "Patriots of Denmark" walichoma moto nakala ya Qur'ani mbele ya ubalozi wa Iraq na kisha mbele ya balozi za Misri na Uturuki huko katika mji mkuu, Copenhagen.
Vitendo hivyo vya ukatili vimekemewa pia na Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambaye ametangaza mshikamano wake na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, na kulaani hatua yoyote inayochochea chuki dhidi ya Uislamu na inayoweza kuongeza mivutano katika jamii.
Siku ya Jumatatu (Julai 31), Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, katika kikao cha 18 kisicho cha kawaida cha mawaziri wa mambo ya nje wa jumuiya hiyo, kilichoandaliwa kwa ajili ya kuchunguza kudhalilishwa Qur'ani Tukufu nchini Sweden na Denmark, kilitoa taarifa muhimu kuhusu hatua madhubuti zinazopaswa kuchukuliwa na Ulimwengu wa Kiislamu ili kukabiliana na vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na unyanyasaji dhidi ya Waislamu na maadili ya dini za mbinguni.