Iran na Algeria zasisitiza kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kimataifa
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran na mwenzake wa Algeria wamesisitiza udharura wa kustawishwa uhusiano wa kiuchumi, kieneo na kimataifa wa pande mbili.
Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran amewaambia waandishi habari baada ya kikao cha pamoja na mwenzake wa Algeria mjini Tehran, kuwa pande mbili zimebadilishana mawazo kuhusu suala la kustawisha uhusiano wa kiuchumi, kieneo na kimataifa, na kufufua kamisheni ya kiuchumi, safari za meli kati ya nchi hizo mbili, na ushirikiano katika uwanja wa elimu.
Qalibaf pia amesisitiza ushirikiano wa pamoja kati ya mabunge ya Iran na Algeria kupitia makundi ya kirafiki ya mabunge ya nchi hizo mbili pamoja na muungano wa mabunge ya nchi za Kiislamu na kusema kuwa, kustawishwa uhusiano huo kunaweza kurahisisha mipango ya kustawisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu huko barani Ulaya katika siku hizi kunapaswa kupigwa vita kali na wakuu wa mabunge ya nchi za Kiislamu.

Kwa upande wake, Ibrahim Boughali, Spika wa Bunge la Algeria amesema katika mkutano huo na waandishi wa habari kwamba, Algeria inalipa heshima kubwa suala la kustawisha uhusiano na nchi rafiki na ndugu ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Spika wa Bunge la Algeria amesisitiza udharura wa kupanuliwa ushirikiano na Iran katika nyuga mbalimbali.