Iran, nchi inayowajibika katika Mashariki ya Kati
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa wananchi wa Iran daima wamekuwa wakitaka kuwa ya uhusiano mzuri na majirani na nchi zote duniani hususan baada ya kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini.
Rais Rouhani aliyasema hayo jana jioni katika hadhara ya mabalozi wa nchi za kigeni na wawakilishi wa jumuiya za kimataifa nchini Iran na kuongeza kuwa miaka 37 iliyopita wananchi wa Iran walifanya mapinduzi makubwa kwa ajili ya kutaka kujitawala na kuwa huru na wakapata ushindi licha ya upinzani wa madola ya kibeberu duniani. Amesema kwamba tangu baada ya ushindi huo Iran ilitaka kuwa na uhusiano mzuri na nchi zote duniani. Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa kushindwa kwa mpango wa kueneza hofu kuhusu Iran kote ulimwenguni ndiyo matunda makubwa zaidi ya makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 maarufuku kwa kifupi kama JCPOA.
Rais Rouhani amekadhibisha madai kuwa Iran inataka kulidhibiti eneo la Mashariki ya Kati na kusema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikodolei jicho nchi yoyote wana haiingilii mambo ya ndani ya nchi nyingine.
Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalisimama juu ya msingi wa mafundisho ya Uislamu na kwa mujibu wa mtazamo wa kuishi pamoja kwa amani, udugu na urafiki na mataifa mengine. Sambamba na kulinda misingi yake, mapinduzi hayo pia yanawajibika kuhusu matukio yote ya kieneo na kimataifa. Iran inaimarisha uwezo wake wa kijihami katika fremu ya maadili ya Kiislamu na kibinadamu na inatumia uwezo wake kwa ajili ya kuimarisha amani na usalama.
Ikiwa nguvu kubwa katika eneo la Mashariki ya Kati, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiwezi kunyamazia kimya na kupuuza matukio ya eneo hilo na imekuwa mstari wa mbele katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo mbalimbali. Kwa msingi huo nafasi na mchango wa Iran katika mapambano dhidi ya ugaidi kama changamoto kubwa zaidi ya nchi za Mashariki ya Kati, si kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine bali kama alivyosema Rais Rouhani, mapambano halisi dhidi ya ugaidi na kurejesha amani na utulivu katika eneo la Mashariki ya Kati vina umuhimu mkubwa kwa Iran na kwamba Tehran imeazimia vilivyo kupambana na ugaidi na kukomesha machafuko katika eneo hilo. Hii ni pamoja na kuwa mchango wa Iran katika mapambano dhidi ya makundi katika nchi za Syria na Iraq umetokana na mwaliko na mwito wa nchi husika. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, sharti la kushinda vita dhidi ya ugaidi ni kushirikiana nchi zote katika kupambana na maovu hayo.
Ukweli ni kwamba juhudi kubwa za Iran katika vita dhidi ya ugaidi na ushirikiano wake wa kutoa ushauri kwa nchi za Iraq na Syria katika uwanja huo ni sehemu ya kuwajibika kwa Tehran kuhusu masuala muhimu ya kieneo na kimataifa na vilevile kutokana na uzoefu mchungu wa Jamhuri ya Kiislamu ambayo hadi sasa imepoteza raia wake elfu 17 kutokana na mashambulizi ya kigaidi. Vilevile inapaswa kueleweka kuwa shari ya makundi ya kigaidi kama lile la Daesh ni balaa kwa walimwengu wote na wala haiishi katika nchi za Syria na Iraq. Mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na kundi la Daesh nchini Ufaransa ni mfano wa ukweli huo.
Iran daima imekuwa ikitangaza kuwa iko tayari kushirikiana na nchi zote katika kuimarisha amani na utulivu na hilo ndilo lililosisitizwa tena na Rais Rouhani katika hobuta yake mbele ya mabalozi wa nchi za kigeni na wawakilishi wa jumuiya za kimataifa katika sherehe ya maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yanazofikia kileleleni hii leo.