Rais Raisi: Vita havina nafasi katika miongozo ya kijeshi ya Iran
Rais Ebrahim Raisi amesema: Vita havina nafasi katika miongozo ya kijeshi ya Iran, lakini kudumisha utayarifu wa kijeshi kwa muelekeo wa kujihami ni sera ya Jamhuri ya Kiislamu isiyo na shaka yoyote.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran Press, Seyed Ebrahim Raisi, ameeleza hayo leo katika gwaride la vikosi vya ulinzi kwa mnasaba wa Wiki ya Kujihami Kutakatifu na akaongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ni kigezo cha utawala unaochanganya masuala ya kiroho na uongozi unaotokana na ridhaa ya watu na inaweza kuwafunza watu wa eneo kwamba kinachomlazimisha adui arudi nyuma si kusalimu amri, kuyumba na kumridhia, bali ni kuonyesha muqawama na kusimama imara.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: tofauti na vikosi vya kijeshi vya kigeni ambavyo uwepo wao huzua matatizo na kusababisha migogoro, uwepo wa vikosi vya Iran katika eneo na Ghuba ya Uajemi kunaleta amani na usalama.
Raisi amesisitiza kwa kusema: uwezo na nguvu za vikosi vya ulinzi na uungaji mkono wa wananchi umewafanya maadui wasizungumze chochote kuhusu kuanzisha uchokozi na uvamizi wa kijeshi, na chaguo hilo limefutwa kwenye misamiati yao.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa:mpango wa adui wa kuitenga Iran umefeli, na kwa nguvu na kusimama imara jeshi na wananchi, mpango wa adui wa kuwakatisha tamaa wananchi pia umefeli.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, vikosi vya ulinzi vimekuwa na vitaendelea kuwa tayari kushirikiana na nchi zote za eneo kwa ajili ya kujenga hali ya kuaminiana na kupeana hakikisho, na vinatoa mkono wa uraifiki kwa vikosi vya ulinzi vya nchi za eneo ili kuliondolea eneo hili na Ghuba ya Uajemi uhitaji wa kuwepo kwa maajinabi na kudhaminiwa usalama wa eneo hili na vikosi vya ukanda huu.
Aidha, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa, kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni hakuziletei usalama nchi za eneo na akabainisha kwamba: "watu wa mataifa ya eneo hili wanauchukia utawala wa Kizayuni na kuanzisha uhusiano na utawala huo ghasibu ni kulichoma jambia la mgongo taifa la Palestina na mhimili wa Muqawama".
Leo Ijumaa, Septemba 22, 2023, inasadifiana na kumbukumbu ya siku vilipoanza vita vya kulazimishwa vya utawala wa Baath wa Iraq dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mnamo Shahrivar 31, 1359 (Septemba 1980), jeshi vamizi la utawala wa Saddam (dikteta mwendazake wa Iraq) lilianzisha mashambulio makubwa dhidi ya Iran kwa kutumia kila aina ya zana za kivita kwa dhana kwamba lingeweza kuiteka Tehran ndani ya wiki moja.
Shahrivar 31 katika kaenda ya Iran ni mwanzo wa Wiki ya Kujihami Kutakatifu, ambapo ndani ya wiki hii, hufanyika mbalimbali katika kila pembe ya Iran ya Kiislamu.../