Sep 26, 2023 12:45 UTC
  • Idadi ya watalii wanaokuja Iran yaongezeka kwa asilimia 38

Naibu Waziri wa Turathi za Kitamaduni, Utalii na Sanaa wa Iran amesema watalii wa kigeni zaidi ya milioni 3.3 waliitembelea Jamhuri ya Kiislamu katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa Kiirani 1402 (Machi 21-Septemba 22).

Ali-Asghar Shalbafian amesema hayo katika kikao na waandishi wa habari hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, idadi hiyo ya watalii walioizuru Iran inaashiria ongezeko la asilimia 38 katika kipindi hicho cha miezi sita ya kwanza ya kalenda ya Hijria Shamsia.

Amesema idadi ya watalii wa kigeni wanaokuja hapa nchini Iran imeongezeka licha ya matukio ya kisiasa na kijeshi yanayoshuhudiwa katika jirani za Azerbaijan na Afghanistan.

Shalbafian amebainisha kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalenga kuongeza idadi ya watalii wanaoitembelea nchi hii hadi milioni 15 kwa mwaka.

Naibu Waziri wa Turathi za Kitamaduni, Utalii na Sanaa wa Iran ameongeza kuwa, programu zaidi ya 130 za kitalii zinatazamiwa kufanyika katika miji zaidi ya 60 ya Iran, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Mei mwaka huu, Shirika la Kimataifa la Utalii la Umoja wa Mataifa (UNWTO) lilisema zaidi ya watalii milioni 4.1 waliitembelea Iran mwaka jana 2022, hilo likiwa ni ongezeko la asilimia 315, ikilinganishwa na mwaka juzi 2021.

Iran ni nchi yenye ustaarabu mkongwe na hivyo ina vivutio vingi vya kitalii kwa wapendao historia. Aidha Iran ina vivutio vingi ya Kiislamu hasa maeneo ya ziara ambayo hutumbelewa na Waislamu kama vile Haram Takatifu ya Imam Ridha AS mjini Mashhad kaskazini mashariki mwa Iran na Haram Takatifu ya Bibi Maasuma SA katika mji wa Qum kusini mwa Tehran.

Tags