Mkuu wa AEOI: Iran haina nia ya kuunda silaha za nyuklia
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema: Iran haina nia ya kuunda silaha za nyuklia na inachofuatilia siku zote ni nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani.
Kongamano la 37 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu lenye kaulimbiu ya "Ushirikiano wa Kiislamu ili kufikia thamani za pamoja" linafanyika hapa nchini kwa kushirikisha wanazuoni na wasomi zaidi ya elfu tatu kutoka nchi 41 duniani.
Baaadhi ya wageni wanaoshiriki katika Kongamano hilo la 37 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu jana Ijumaatatu walitembelea kinu cha utafiti cha Shahid Fakhrizadeh mjini Tehran na maabara za uzalishaji wa dawa za miale katika Shirika la Nishati ya Atomiki.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran Press, katika ziara hiyo, Mohammad Eslami, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesema, mafanikio ya teknolojia ya nyuklia ya Iran yanalenga kuleta amani na kutoa huduma kwa wanadamu na akabainisha kuwa: Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran linachukuliwa kuwa moja ya mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu na sasa limekuwa moja ya fakhari kubwa kwa Iran na hata kwa Ulimwengu wa Kiislamu.
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesisitiza kuwa: shughuli zote zinafanywa kwa kuzingatia viwango na kanuni za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.
Eslami ameashiria vikwazo vya maadui dhidi ya Iran na kusisitiza kwamba Iran inapinga kila aina ya ubeberu na ukiritimba wa sayansi na teknolojia, na akaongezea kwa kusema: "tumeweza kuzima athari za vikwazo hivyo kwa juhudi za wataalamu wetu wa ndani".../