Abdollahian: Kuendelea mashambulizi ya Israel huko Gaza yumkini kukapanua wigo wa mapigano
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mazungumzo yake na Amir Qatar kwamba: "Iwapo mashambulio ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya raia wa Palestina na watu wasio na ulinzi katika ukanda wa Gaza yataendelea, hakuna mtu anayeweza kudhibiti hali hiyo au kutoa dhamana na kutopanuka zaidi migogoro huo."
Hossein Amir Abdollahian amemwambia Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, mjini Doha kuwa: Marekani ambayo inazishauri pande nyingine kujizuia, yenyewe haiheshimu ushauri huo na imezidisha himaya na misaada yake ya pande zote kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Wale wenye nia ya kuzuia kupanuka zaidi vita na mgogoro huu, wanalazimika kuzuia mashambulizi ya hivi sasa ya utawala wa Kizayuni dhidi ya raia na watu wa Palestina katika ukanda wa Ghaza.
Amir Abdollahian ameashiria pia mazungumzo yake na maafisa wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) huko Beirut na Doha na kusema: Maafisa wa harakati hiyo wamesisitiza kuwa, kutokana na mtazamo wa Kiislamu na kibinadamu, wanalipa kipaumbele suala la mateka wa kiraia, na kwamba iwapo kutatayarihwa mazingira yanayofaa, watachukua hatua zinazohitajika katika uwanja huu.
Kwa upande wake, Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani, Amir wa Qatar pia ametaja hali ya watu wa Ghaza kuwa ni ya kutia wasiwasi na kusema: “Kipaumbele ni kusimamisha jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza, na kwamba msimamo wa Doha kuhusu Palestina hautabadilika."
Utawala bandia wa Israel, ambao juhudi zake za kusimamisha operesheni za Muqawama katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu zimeshindwa hadi sasa, na viongozi wa utawala huo bado wako katika mshtuko mkubwa wa kipigo cha Kimbunga cha al Aqsa, unaendelea kuwalenga raia wa Palestina na kuwalazimisha kuondoka Gaza.