IRGC: Kushindwa Israel kutaleta amani na usalama duniani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i104502-irgc_kushindwa_israel_kutaleta_amani_na_usalama_duniani
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) sambamba na kulaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza amesema kuwa, kushindwa utawala wa Kizayuni na kuporomoka kwa Marekani, ni chanzo cha kupatikana amani na usalama duniani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 08, 2023 02:54 UTC
  • IRGC: Kushindwa Israel kutaleta amani na usalama duniani

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) sambamba na kulaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza amesema kuwa, kushindwa utawala wa Kizayuni na kuporomoka kwa Marekani, ni chanzo cha kupatikana amani na usalama duniani.

Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la SEPAH alisema hayo jana Jumanne hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa: Mwezi mmoja baada ya utawala wa Israel kwa uungaji mkono wa Marekani kuanzisha mashambulizi ya kinyama dhidi ya Wapalestina wa Gaza, watu zaidi ya 10,000 wasio na hatia wameuawa.

Salami amesema: Hii leo, utawala wa Kizayuni ni kama jino bovu lililooza ambalo limeachana na mzizi wake, na limeanza kuhisika linaporomoka kwa kasi; na Wamarekani pia wameanza kugundua kuporomoka kwa taswira na itibari yao machoni pa dunia.

Kamanda Salami ameongeza kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel, si tu kwamba umepata pigo kubwa bali pia umeshindwa kwa fedheha na wanamuqawama wa Palestina.

Ukatili wa Wazayuni katika Ukanda wa Gaza

Kuangamizwa Wazayuni zaidi ya 1,500 wakiwemo mamia ya wanajeshi ya utawala huo ghasibu, ni sehemu ndogo ya matunda ya Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ya wanamapambano wa Palestina iliyoanza Oktoba 7.

Jenerali Salami amebainisha kuwa, kushindwa Wazayuni katika Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ni moja ya vipigo vikubwa na vya aina yake ambavyo havijawahi kushuhudiwa, na ambavyo vimeziyumbisha Marekani na Israel.

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa imeyumbisha mfumo wa ubeberu wa maadui.