Nov 12, 2023 02:56 UTC
  • Iran na China zakubaliana kuanzisha kituo cha pamoja cha mafunzo ya teknolojia mpya

Wakuu wa Idara za Mafunzo za Wizara za Sayansi, Utafiti na Teknolojia za Iran na China wamekubaliana juu ya kuanzishwa kituo cha pamoja cha utoaji mafunzo ya kiufundi na kitaalamu na mafunzo ya teknolojia mpya.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Mkutano Mkuu wa 42 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO unafanyika Paris, mji mkuu wa Ufaransa, kuanzia Novemba 7 hadi 12.
 
Kando ya mkutano huo, Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya Wizara ya Sayansi, Utafiti na Teknolojia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana na kufanya mazungumzo na Wakuu wa Idara za Mafunzo za nchi mbalimbali.
 
Katika moja ya mikutano aliyofanya pembeni ya mkutano huo mkuu wa UNESCO, Ghasem Amouabedini, Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya Wizara ya Sayansi, Utafiti na Teknolojia ya Iran amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Idara ya Mafunzo kutoka China.

Katika mazungumzo hayo, wawili hao wamefikia makubaliano juu ya pendekezo la kuanzishwa kituo cha pamoja cha mafunzo ya ufundi na utaalamu na mafunzo ya teknolojia mpya, na ikaamuliwa kuwa katika siku chache zijazo, wawakilishi wa elimu ya juu wa pande mbili watachukua hatua zinazohitajika kwa ajili ya kusaini hati za makubaliano za utoaji mafunzo na utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa.

 
Katika muendelezo wa mikutano aliyofanya na maafisa wa elimu ya juu wa nchi washiriki wa Mkutano Mkuu wa 42 wa UNESCO, Amouabedini amekutana pia na Waziri wa Elimu ya Juu, Utafiti na Teknolojia wa Oman, Rahmah bint Ebrahim al-Mahruqa pamoja na Naibu wake wa Elimu.
 
Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili zilibadilishana mawazo kuhusu ushirikiano wa kielimu na ikaamuliwa kuwa Iran na Oman zitaanzisha vituo vya pamoja vya mafunzo ya ufundi na utaalamu kwa wanafunzi na wanachuo wa nchi mbili.../

 

Tags