Kamanda Fadavi: Nguvu za wananchi wa Palestina zimeifanya dunia kuemewa
Kaimu Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) amesema kuwa, nguvu zilizooneshwa na wananchi wa Palestina katika vita vya hivi sasa vya Ghaza zimeishangaza dunia na kuifanya iemewe, na ijiulize, nguvu hizi wamezitoa wapi wananchi hawa wa Palestina.
Brigedia Jenerali Ali Fadavi ameongeza kuwa, mawe ndiyo silaha pekee waliyokuwa nayo Wapalestina huko nyuma, lakini leo hii Wapalestina hao wamejizatiti kwa silaha ambazo zimeyafanya madola makubwa duniani yaemewe.
Amesema: Operesheni ya #Kimbunga_cha_al-Aqsa imetoa pigo kubwa kwa Israel kiasi kwamba madola ya shari yote duniani yalifanya haraka kujipeleka kwenye ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni huku yakihaha kutafuta njia za kuzuia kusambaratika kikamilifu utawala wa Kizayuni; mtenda jinai.
Ameongeza kuwa, Marekani na nchi za Ulaya zinashirikiana kikamilifu na utawala wa Kizayuni kwenye vita vya Ghaza, lakini hadi hivi sasa zimeshindwa kupata picha angalau moja ya mwanamapambano wa Palestina aliyeuawa shahidi.

Kaimu wa Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amesisitiza kuwa, wananchi wa Ghaza wameunda hamasa kubwa katika vita vya hivi sasa kiasi kwamba, utawala wa Kizayuni na nchi za Magharibi ndizo zilizoomba kusimamishwa vita kwani ziko kwenye mashinikizo makubwa ndani ya nchi zao na kwenye medani za vita.
Brigedia Jenerali Fadavi ameongeza kuwa, nguvu za kambi ya muqawama katika eneo hili ni kubwa na kuna wakati Yemen ilikuwa nchi maskini zaidi kati ya wanachama wa kambi ya muqawama lakini leo hii Wayemen wana nguvu kiasi kwamba, wana uwezo wa kutungua ndege ya kisasa kabisa ya Marekani isiyo na rubani.
Hatimaye na baada ya kupita siku 48 za vita vya kijinai na kikatili vya Israel dhidi ya wananchi wa Ghaza, utawala huo wa Kizayuni umelazimika kukubali kusimamisha vita kwa muda wa siku nne kwa masharti ya wanamapambano wa Palestina ikiwa ni pamoja na kubadilishana mateka ambapo Israel itaachilia huru Wapalestina 150 mkabala wa kuachiliwa huru Wazayuni 50 tu walioko mikononi mwa wanamapambano wa Palestina.