Raisi: Msingi wa uungaji mkono wa Iran kwa Palestina ni Katiba
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ndio msingi wa taifa hili kuiunga mkono Palestina na Ukanda wa Gaza ambao hivi sasa unakabiliwa na mashambulizi ya Wazayuni.
Rais Ebrahim Raisi amesema hayo leo Jumapili akihutubia Kongamano la Kitaifa la Uwajibikaji na Utekelezaji wa Katiba hapa mjini Tehran na kusisitiza kuwa, kuwaunga mkono wanaodhulumiwa ni katika misingi mikuu ya Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu.
Sayyid Raisi ameeleza bayana kuwa, kuliunga mkono taifa la Palestina limekuwa na limeendelea kuwa suala kuu hapa nchini Iran, tangu baada ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979.
Amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu kamwe haitaacha kufungamana na msingi huo muhimu wa Katiba, licha ya misimamo ya baadhi ya madola katika eneo.
Rais Raisi amegusia kauli ya msomi mmoja mashuhuri wa sheria wa Afrika aliyesema kuwa Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ni mchanganyiko wa demokrasia na thamani za maadili na kubainisha kuwa, Katiba ya Iran ndiyo bora zaidi miongoni mwa nchi za dunia.
Amesema licha ya mikusanyiko na maandamano dhidi ya Israel kuendelea kushuhudiwa katika pembe mbalimbali za dunia, lakini utawala huo unaendelea kumwaga damu za watoto na wanawake wa Kipalestina
Ameashiria mauaji ya watoto zaidi ya 6,000 katika hujuma na mashambulizi ya kinyama ya Israel dhidi ya Gaza na kusema kuwa, utawala wa Kizayuni utasambaratishwa na kisasi kitakatifu cha damu za watoto hao.
Rais wa Iran amesema mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza ambayo mpaka sasa yamepelekea kuuawa shahidi watu 15,200, yamefichua dhati ya ubaguzi, ukatili, na dhulma ya utawala huo dhidi ya Wapalestina.
"Hatuna shaka kwamba kisasi kitakatifu kitaibuka kutokana na damu za watoto 6,000 ambao wameuawa shahidi kidhulma, na (kisasi hicho) kitautokomeza utawala katili na bandia," ameongeza Rais Raisi.