Kikosi cha 93 cha Manowari za Jeshi la Iran charejea nyumbani baada ya kulinda doria katika Bahari ya Sham
(last modified Fri, 08 Dec 2023 07:43:52 GMT )
Dec 08, 2023 07:43 UTC
  • Kikosi cha 93 cha Manowari za Jeshi la Iran charejea nyumbani baada ya kulinda doria katika Bahari ya Sham

Kikosi cha 93 cha Kivita cha Manowari za Kikosi cha Kimkakati cha Wanamaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kikiongozwa na manowari ya Jamaran zimerejea nyumbani baada ya siku 102 za kutekeleza jukumu la kuhakikisha usalama wa meli za mafuta na za kibiashara za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Bahari ya Sham na Ghuba ya Aden.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, msafara wa meli hizo ambao umesafiri umbali wa kilomita elfu 13 katika bahari ya wazi na ya kimataifa, ulirejea katika bandari za Iran Alhamisi na kukaribishwa na Admeri Babak Baloch, Naibu Mratibu wa Kikosi cha Kimkakati cha Wanamaji cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, makamanda wa kijeshi na familia za wanamaji hao.

Tangu mwaka 2009, wakati  Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Iran, ambaye pia ni Kiongozi Muadhamu wa Mapinaduzi ya Kiislamu,  aliamuru Jeshi la Wanamaji la Iran na meli za kivita za Iran ziwe zinafika katika maeneo ya bahari za mbali, Jeshi la Wanamaji la Iran limekuwa likituma manowari zake katika operesheni za kulinda doria katika  Ghuba ya Aden,  Bahari ya Sham na Bahari ya Hindi ili kusindikiza meli za kibiashara na za kubeba mafuta za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi nyinginezo. Eneo hilo kwa muda mrefu limekuwa likikumbwa na hujuma za maharamia baharini. Shirika la Umoja wa Mataifa la Usafiri wa Majini (IMO) limepongeza juhudi za Iran za kudumisha usalama baharini na kukabiliana na maharamia katika eneo la karibu na pwani ya Somalia.

Mwezi Mei mwaka huu Msafara wa 86 wa Meli za Kivita za Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulirejea nchini baada ya safari ya kuzunguka dunia kama sehemu ya juhudi za Jamhuri ya Kiislamu za kupanua uwepo wake kijeshi katika bahari za mbali.

Msafara huo wa Jeshi la Wanamaji la Iran, ulijumuisha meli ya kivita ya Dena iliyotengenezwa nchini ambayo ina uwezo mkubwa wa kuharibu manowari za adui na hali kadhalika meli ya kivita ya Makran inayosheheni zana za kivita na vifaa vingine muhimu vinavyotumika katika oparesheni za kijeshi majini.

Manowari hizo zilisafiri masafa ya kilomita 63,000 baharini katika muda wa miezi minane na kuzunguka dunia kwa nyuzi 360.