Dec 13, 2023 02:47 UTC
  • Tehran yalaani vikwazo vya EU dhidi ya Wizara ya Ulinzi ya Iran

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imekosoa vikali hatua ya Umoja wa Ulaya ya kuiwekea vikwazo Wizara ya Ulinzi ya nchi hii kwa madai bandia kuwa Jamhuri ya Kiislamu imeipa Russia ndege zisizo na rubani (droni) eti kwa ajili ya kutumika vitani huko Ukraine.

Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza katika taarifa ya jana Jumanne kuwa, madai eti Iran imeipa Russia ndege zisizo na rubani kwa ajili ya kutumika vitani huko Ukraine hayana ukweli wowote.

Kan'ani ameongeza kuwa, inasikitisha kwamba nchi ambazo ndizo zinazouza pakubwa silaha na zana za kijeshi kwa upande mmoja katika vita vya Ukraine zinafanya mikakati ya kuzipotosha fikra za walimwengu kwa kueneza taarifa na madai ya  uwongo. 

Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haipendelee upande wowote katika vita hivyo. 

Juzi Jumatatu, Baraza la Ulaya lilitangaza vikwazo dhidi ya shakhsia 6 na taasisi 5 zinazofungamana na sekta ya ulinzi ya Iran kwa madai hayo yasiyo na msingi eti Iran imeipa Russia droni za kutumia katika vita vyake na Ukraine.

Kabla ya hapo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aliyataja madai ya jarida la Wall Street Journal la Marekani kwamba Iran na Russia zinajenga kiwanda chenye uwezo wa kuunda ndege zisizo na rubani (droni) elfu sita kwa ajili ya kutumika vitani huko Ukraine kuwa ni ya uongo.

EU imetangaza vikwazo dhidi ya Iran katika hali ambayo, hivi karibuni, Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya alisema kuwa, nchi kadhaa za Ulaya zimetuma maombi yao ya kutaka kuuziwa ndege zisizo na rubani za Iran.

 

Tags