Dec 18, 2023 06:12 UTC
  • Uungaji mkono usio na kikomo wa US na UK kwa utawala wa Kizayuni; kuanzia misaada ya kila hali mpaka uwekaji vikwazo dhidi ya Muqawama

Serikali za Marekani na Uingereza zinazojinasibu kuwa watetezi wa haki za binadamu, mara hii zimeendeleza uungaji mkono wao kwa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza kwa kuwawekea vikwazo vipya makamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

Takribani siku 70 zimepita tangu utawala katili wa Kizayuni ulipoanzisha vita dhidi ya Gaza. Idadi ya waliouawa shahidi na kujeruhiwa katika vita hivi imeshafikia karibu watu elfu 70. Walimwengu katika nchi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Marekani na Uingereza, wamelaani na wanaendelea kulaani jinai hizo.
Maandamano ya kuunga mkono Palestina yaliyofanyika Marekani

Wakati baadhi ya serikali zenye misimamo huru na taasisi kadhaa za kimataifa na pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wametangaza rasmi kuwa yanayoendelea kujiri Gaza ni mauaji ya kimbari, tawala kadhaa za Magharibi hususan Marekani na Uingereza zimekuwa zikitoa misaada na uungaji mkono wa kila aina kwa utawala dhalimu wa Kizayuni katika vita unavyoendeleza dhidi ya Ukanda wa Gaza.

Mbali na misaada na uungaji mkono wa kijeshi, nchi hizo zimeandaa mazingira ya kuendelezwa jinai ya mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza kwa kuitumia vibaya na kisiasa haki ya kura ya veto katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa; na kimsingi, wao ni washirika wa jinai zinazofanywa na Wazayuni.
Sasa hivi Marekani na Uingereza zimeonyesha namna nyingine ya uungaji mkono wao kwa utawala wa Kizayuni kwa kuwawekea vikwazo makamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC). Siku ya Ijumaa tarehe 15 Disemba serikali ya Uingereza ilimuwekea vikwazo Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds cha IRGC na makamanda wengine sita waandamizi wa jeshi hilo kwa madai ya kushirikiana na harakati za Muqawama wa Palestina za HAMAS na Jihadul-Islami.
Mbali na US na UK, EU na Ujerumani pia zinaunga mkono mauaji ya kimbari ya Wapalestina wa Gaza

Uingereza imewajumuisha pia kwenye orodha hiyo ya vikwazo Khalid Qadoumi na Nasser Abu Sharif, wawakilishi wa Hamas na Jihadul-Islami hapa nchini Iran. Katika upande mwingine, Wizara ya Fedha ya Marekani nayo pia siku hiyohiyo ilitangaza vikwazo dhidi ya makamanda kadhaa wa Kikosi cha Quds kwa kisingizio hichohicho.

Uwekaji vikwazo hivyo unamaanisha kwamba, mantiki ya ubabe na utumiaji nguvu na mabavu ndiyo inayotawala mfumo wa dunia, kwa sababu Marekani na Uingereza zinauunga mkono kwa kila hali utawala wa Kizayuni na kuzuia kupitishwa azimio lolote katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kusimamisha vita huko Gaza, lakini mkabala wa hayo zinawawekea vikwazo makamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa madai ya kuziunga mkono harakati za Hamas na Jihadul-Islami.
Nukta nyengine ni kwamba, madai hayo yanatolewa katika hali ambayo tangu mwaka 2007 hadi sasa, Gaza imewekewa mzingiro wa kila upande na utawala dhalimu wa Kizayuni, kiasi kwamba haiwezekani hata kupeleka misaada ya kibinadamu katika eneo hilo, seuze misaada ya kijeshi.

Mienendo ya Washington na London inaonyesha dhahir shahir kuwa mauaji ya kimbari ya Waislamu ni suala linaloungwa mkono na nchi hizo.

Katika upande mwingine, mienendo hii inaonesha kuwa, vita vya Gaza, kama alivyosisitiza mara kadhaa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, si vita kati ya Hamas na utawala wa Kizayuni, bali ni vita vya Magharibi dhidi ya Waislamu.
Kuwawekea vikwazo makamanda na maafisa wa Muqawama ni kielelezo cha wazi cha kuchanganyikiwa na kutoweza utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake kukabiliana na Muqawama unaoongozwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Nasser Kan'ani amelaani vikwazo vilivyowekwa na Marekani na Uingereza dhidi ya Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds cha IRGC na kusisitiza kwamba: Iran na vikosi vyake rasmi vya ulinzi na vya kisheria kikiwemo kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu daima itaendelea kuwa jinamizi kwa magenge ya kigaidi na tawala zinazoyaunga mkono.../

 

Tags