Azma ya Tehran na Islamabad ya kuimarisha uhusiano wao katika nyuga mbalimbali
(last modified Mon, 01 Jan 2024 08:00:57 GMT )
Jan 01, 2024 08:00 UTC
  • Azma ya Tehran na Islamabad ya kuimarisha uhusiano wao katika nyuga mbalimbali

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Pakistan ameeleza kuridhishwa kwake na mwenendo unaokua wa uhusiano kati ya nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Balozi Mumtaz Zahra Baloch amesema, kutiwa saini mpango wa ushirikiano wa kibiashara wa miaka mitano kati ya pande hizo mbili mwaka uliopita wa 2023 kuwa ni hatua muhimu katika kufikia kiwango cha mabadilishano ya kibiashara kati ya Pakistan na Iran cha dola bilioni tano kwa mwaka.

Akizungumza na waandishi wa habari, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Pakistan, ameashiria nafasi muhimu ya kusainiwa makubaliano ya pande mbili katika kuongeza ushirikiano wa kiuchumi kati ya Islamabad na Tehran, na kubainisha kwamba, kwa ufuatiliaji wa viongozi na juhudi za wafanyabiashara na wawekezaji kutoka pande zote mbili; katika siku zijazo, kiasi cha mabadilishano ya kibiiashara kati ya nchi hizo mbili kitafikia karibu dola bilioni 5 kwa mwaka.

Uhusiano wa Iran na Pakistan ambao una historia ndefu ya umri wa uhuru wa Pakistan umekuwa ukiongezeka katika miaka ya hivi karibuni katika sekta mbalimbali. Pakistan ikiwa moja ya nchi jirani na Iran, ina mpaka mrefu zaidi wa pamoja na Iran baada ya Iraq, ukiwa na zaidi ya kilomita 900 kwa upande wa nchi kavu. Hata hivyo, kiasi cha mabadilishano ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili hakijawahi kuwa katika kiwango kinachotarajiwa na maafisa wa pande zote mbili, na kawaida kimebakia katika kiwango cha dola bilioni moja kwa mwaka. Inaonekana kuwa, kufanana kwa bidhaa za nchi mbili zinazouzwa nje ya nchi hasa katika sekta ya bidhaa za kilimo na viwanda inahesabiwa kuwa moja ya sababu za kuzorota kwa ustawi katika mabadilishano ya pande mbili.

Pamoja na hayo, thamani ya mabadilishano kati ya nchi hizo mbili katika mwaka uliopita ilizidi dola bilioni mbili kwa mwaka kwa mara ya kwanza kutokana na juhudi za maafisa wa nchi hizo mbili, na inatabiriwa kwamba kwa kuweko azma ya viongozi na maafisa wa nchi mbili hizi ya kuongeza ushirikiano wa kibiashara, hasa kusaidia kurahisisha na kuhuisha biashara ya mipakani katika katika siku za usoni, kiwango cha biashara baina ya nchi hizo mbili kitaongezeka na kufikia tarajio la maafisa wa nchi hizo mbili, yaani hadi dola bilioni tano kwa mwaka.

Kuhusiana na hilo, Hassan Noorian balozi mdogo wa Iran huko Karachi, makao makuu ya mkoa wa Sindh wa Pakistan, amesema: Kuna uwezekano wa kukua kwa biashara kati ya nchi hizo mbili, na kupanua uhusiano huo na kuongeza kuwa, vikwazo kama vile kanali za benki, vikwazo vya forodha na kutotambuliwa kwa wafanyabiashara wa nchi hizo mbili ni mambo ambayo yanapaswa kuondolewa sambamba na kufanyika juhudi zaidi za kuwezesha upanuzi wa mahusiano baina ya nchi hizo mbili.

 

Aidha Hassan Noorian amesema: Kuendelea kwa vikao na mashauriano baina ya viongozi wa nchi hizo mbili na ufuatiliaji wa makubaliano yaliyofikiwa ni jambo muhimu zaidi katika kuongeza kiwango cha mabadilishano kati ya nchi hizo mbili.

Katika mazingira kama haya, kuweko vikao mbalimbali na vingi baina ya viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan katika mwaka uliomalizika jana wa 2023, kikiwemo kikao cha Seyyed Ebrahm Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Waziri Mkuu wa wakati huo wa Pakistan (Shehbaz Sharif) katika eneo la mpakani, ziara ya Kamanda wa Jeshi la Wanamaji wa Iran mjini Islamabad na ziara ya Kamanda Jeshi la Pakistani mjini Tehran ni mambo ambayo yamekuwa na nafasi muhimu katika kupanua uhusiano baina ya nchi mbili hizi za Kiislamu.

Ni jambo lisilo na shaka kuwa, kustawishwa kwa mahusiano ya umma ni sababu nyingine ya ustawi wa uhusiano kati ya nchi hizo na hasa nchi jirani kama vile Iran na Pakistan ili kufikia malengo ya pamoja, na katika suala hili nafasi ya vyombo vya habari vya nchi hizo mbili inachukuliwa kuwa muhimu sana. Kwa sababu hiyo, nchi hizo mbili zilichukua hatua madhubuti katika mwaka uliopita kwa lengo la kuakisi vivutio, uwezo na taswira yao halisi kwa watu wa nchi hizo kwa kutuma wajumbe wa kisayansi, kitamaduni na kidini.

 

Pamoja na hayo yote, Pakistan ikiwa ni jirani ya Mashariki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bado haijatambuliwa vyema na wanaharakati wengi wa masuala ya kiuchumi na wafanyabiashara wa Iran, huku soko la bidhaa za nchi hii ya watu milioni 240 likiwa na uwezo mkubwa. Ni kutokana na sababu hiyo ndio maana, kufahamishwa wanaharakati wa kiuchumi na wafanyabiashara wa Iran na Pakistan kuhusu uwezo wa pande zote mbili, pamoja na kustafidi na diplomasia ya kieneo na kiuchumi, kutaleta matokeo mengi mazuri kwa nchi hizo mbili.

Ni dhahir shahir kwamba, lililo na tija zaidi ni irada ya Islamabad ya kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kati yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hususan mpango wa kusafirishwa gesi ya Iran kuelekea nchini humo. Kwa hivyo inatarajiwa kuwa, maafisa wa serikali ya Pakistan wataharakisha utekelezaji akthari ya hati za makubaliano ya pande mbili ili kujikomboa kutoka kwa mashinikizo kutoka nje na wakati huo kutekelezwa matakwa ya wananchi wa pande mbili.

Tags