Jan 09, 2024 07:52 UTC
  • de Volkskrant: Uholanzi ilihusika katika hujuma ya virusi vya Stuxnet ya Marekani, Israel dhidi ya Iran

Gazeti la de Volkskrant la Uholanzi limeripoti kuwa, raia mmoja wa nchi hiyo alihusika moja kwa moja katika operesheni ya Marekani na Wazayuni ya kuhujumu kituo cha nyuklia cha Natanz nchini Iran.

Gazeti hilo limeandika katika ripoti yake kwamba, mwaka 2007, raia mmoja wa Uholanzi alikuwa na nafasi muhimu katika mpango wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel wa kuhujumu miundombinu ya kurutubisha madini ya Uranium ya Natanz nchini Iran bila ya serikali ya nchi hiyo kujua.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, raia huyu wa Uholanzi, ambaye jina lake ni "Erik van Saben", amekuwa na jukumu kubwa katika kuchafua mifumo ya udhibiti ya kituo cha kurutubisha madini ya uranium cha Natanz nchini Iran kwa virusi vya "Stuxnet"; Hatua iliyopelekea kusimama kwa muda miradi ya nyuklia ya Iran.

Raia huyo wa Uholanzi, ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 36, aliuawa katika ajali ya gari karibu na nyumbani kwake huko Dubai miaka 2 baada ya wadhifa wake.

Gazeti la Uholanzi la de Volkskrant limekuwa likichunguza operesheni hiyo ya hujuma kwa muda wa miaka 2 iliyopita na limewahoji watu kadhaa, wakiwemo watu 19 wanaofanya kazi katika Idara za Usalama za Uholanzi.

Stuxnet ni programu haribifu ya kompyuta ambayo iligunduliwa kwa mara ya kwanza tarehe 13 Julai 2010 na programu ya kukabiliana na virusi ya Vba32 AntiVirus.

Inavyoonekana ni kuwa, virusi hivyo vya kompyuta viliundwa na kusambazwa kwa shabaha ya kushambulia vituo vya udhibiti wa miradi ya nyuklia ya Iran, lakini sasa imekuwa hatari inayoonyesha utata na ugumu wa vita vya mtandao.

Tags