Tehran: Iran na Pakistan hazitaruhusu maadui waharibu uhusiano wao wa kindugu
(last modified Sun, 28 Jan 2024 07:54:18 GMT )
Jan 28, 2024 07:54 UTC
  • Tehran: Iran na Pakistan hazitaruhusu maadui waharibu uhusiano wao wa kindugu

Kufuatia shambulio lililowalenga raia wa Pakistan ndani ya Iran, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema Tehran na Islamabad hazitavumilia chokochoko za kuharibu uhusiano wa nchi hizo mbili.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kan'ani amesema "Iran na Pakistan hazitaruhusu maadui waharibu uhusiano wa kindugu wa nchi hizi".

Kauli yake imekuja saa chache baada ya washambuliaji wasiojulikana kuwaua kwa kuwapiga risasi raia tisa wa Pakistan na kuwajeruhi wengine watatu katika kitongoji cha mji wa Saravan katika mkoa wa Sistan na Baluchestan kusini mashariki mwa Iran.

Kwa mujibu wa Naibu Gavana wa mji huo anayehusika na Usalama Alireza Marhamati hujuma hiyo ilifanywa na watu watatu waliokuwa na silaha, ambao walivamia makazi ya raia hao wa Pakistan, na kukimbia eneo la tukio baada ya kusababisha maafa hayo ya kuteketeza roho za watu tisa na kuwajeruhi wengine kadhaa.

Kan'ani amelaani vikali shambulio hilo na kutoa pole kwa serikali ya Pakistan na jamaa wa waliofariki.

Ameongeza kuwa, mamlaka husika za Iran zinaendelea na uchunguzi wao kuhusu tukio hilo.

Jana Jumamosi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Jalil Abbas Jilani, alilaani shambulio hilo, akisema ni njama ya "maadui waliozoeleka" wa nchi hizo yenye lengo la kuvuruga uhusiano wao wa pande zote.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Pakistan alituma salamu za rambirambi pia kwa familia za wahanga, akiitaka serikali ya Iran kuchukua hatua zinazostahili dhidi ya wale waliohusika na shambulio hilo.

Katika siku za karibuni nchi hizo mbili jirani zimeshuhudia mivutano ya mpakani iliyohusiana na operesheni za Iran za kupambana na ugaidi.../

Tags