Mipaka ya Iran na Pakistan kubadilishwa kuwa ya kiuchumi na kiurafiki
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, juhudi zinafanyika kuhakikisha kwamba, mipaka ya nchi yake na Pakistan inabadilika na kuwa ya kiuchumi, amani na urafiki.
Shirika la habari la Tasnim limenukuu Hossein Amir-Abdollahian akisema hayo jana (Jumatano) na kusisitiza kuwa, kutiwa nguvu harakati za kibiashara na mabadilishano ya kiuchumi baina ya Iran na Pakistan ni muhimu sana kwa Jamhuri ya Kiislamu na jitihada kubwa zilizopo hivi sasa ni za kushirikiana kupambana na magenge ya kigaidi yanayotumia vibaya mipaka hiyo na badala yake kuibadilisha kuwa vituo vikuu vya kiuchumi, amani na urafiki baina ya pande mbili.
Vilevile amegusia ziara yake nchini Pakistan na kusema kuwa, wakati wa ziara yake hiyo amefanya mazungumzo mazuri na ya maana na viongozi wa ngazi mbalimbali wa Pakistan.
Jumatatu wiki hii, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alionana na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Pakistan pamoja na mkuu wa jeshi na waziri mkuu wa nchi hiyo ndugu na jirani huko Islamabad.
Akiwa safarini kurejea humu nchini, Hossein Amir-Abdollahian aliwaambia waandishi wa habari mjini Islamabad kwamba, wakati wa mazungumzo yake na wakuu wa ngazi mbalimbali wa Pakistan, kumefikiwa makubaliano ya kuzidisha ushirikiano wa kiuchumi, kibiashara, kiutalii, kinishati na masuala mengine mengi kwa faida ya wananchi wa mataifa haya mawili ya Waislamu.
Aliongeza kuwa, serikali za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan zina makubaliano ambayo yameainishiwa ratiba na muda maalumu wa utekelezaji. Hivi sasa kuna vituo vitano vipya vya mpakani vimefunguliwa baina ya majirani hawa wawili na jitihada zimeongezwa hivi sasa kuhakikisha magenge ya kigaidi hayatumii mipaka ya nchi hizi mbili kuhatarisha amani na usalama.