"US inakiuka Hati ya UN kwa kutishia kuiwekea tena vikwazo Venezuela"
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa vikali hatua ya Marekani ya kutishia kuiwekea upya vikwazo sekta ya mafuta ya Venezuela na kusisitiza kuwa, kkitendo hicho kinakanyaga Hati ya Umoja wa Mataifa na sheria ya kimataifa.
Nasser Kan'ani amesema hayo leo Alkhamisi na kuongeza kuwa, Marekani ingali inaendeleza sera zake za uhasama na uadui dhidi ya nchi zingine duniani kwa kutumia vitisho na vikwazo.
Ameeleza bayana kuwa: Kutumia njia hizo (za vikwazo na vitisho) ni kuingilia moja kwa moja masuala ya ndani ya nchi nyingine na kukiuka Hati ya Umoja wa Mataifa.
Kan'ani amebainisha kuwa, kitendo cha Marekani cha kuamua kutumia vitisho na vikwazo kitayafanya mataifa huru duniani kuungana na kuchukua hatua za kukabiliana na vitendo hivyo vya uingiliaji.
Vikwazo vimeendelea kufanywa kuwa moja ya wenzo wa madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani wa kuleta mashinikizo ya kiuchumi na kisiasa kwa mataifa yanayojitawala na yasiyokubali kuburuzwa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu na nchi hiyo ya Amerika Kusini ni washirika wakuu katika kupambana na vikwazo na mashinikizo ya mabeberu.
Siku ya Jumatatu, Wizara ya Fedha ya Marekani ilitishia kufufua wimbi la vikwazo dhidi ya Venezuela, siku chache baada ya Mahakama ya Juu ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini kushikilia uamuzi wa kumpiga marufuku kiongozi mmoja wa upinzani kushiriki uchaguzi wa rais.