Iran ni miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza duniani katika sekta ya bahari
(last modified Thu, 15 Feb 2024 02:30:22 GMT )
Feb 15, 2024 02:30 UTC
  • Iran ni miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza duniani katika sekta ya bahari

Naibu Waziri wa Barabara na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bandari na Bahari la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kila mwaka meli 40,000 hupita katika bandari za Iran na kuongeza kuwa, Iran ni miongoni mwa nchi 10 bora duniani katika sekta ya bahari.

Ali-Akbar Safaei, Naibu Waziri wa Barabara na Maendeleo ya Miji na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bandari na Bahari la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyasema hayo jana Jumatatu katika kongamano la Uchumi wa Bahari wa Iran. 

Katika kikao hicho aliashiria pwani za kimkakati za Iran katika Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman na Bahari ya Kaspi kaskazini mwa nchi pamoja trafiki kubwa ya meli za kigeni katika  bandari za Iran na kusema, nchi imeshuhudia ustawi mkubwa katika sekta hiyo ambayo inazidi kustawi.

Kutayarishwa hati ya maendeleo ya uchumi wa bahari kama hatua ya mabadiliko katika sera za bahari za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miaka ya hivi karibuni kunaonyesha kuwa, Tehran inaiona bahari kuwa moja ya vipengele muhimu vya maendeleo ya nchi. Kwa sababu hiyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inajaribu kuwa moja ya vitovu muhimu vya usafirishaji wa bidhaa katika eneo la Magharibi mwa Asia na dunia katika siku za usoni, kwa kuzingatia uwezo uliopo na kuongeza vitega uchumi vya kigeni.

Ushirikiano wa pamoja wa Iran, India na Afghanistan kwa ajili ya maendeleo ya bandari ya Chabahar kusini mashariki mwa Iran na uwekezaji mkubwa wa India katika bandari hiyo katika miaka ya hivi karibuni kwa lengo la kufikia masoko ya kikanda, hasa Afghanistan na Asia ya Kati, na kisha Russia na Ulaya vinatathminiwa kuwa hatua muhimu katika mwelekeo huu.

Kwa sababu hiyo, Ali-Akbar Safaei, Naibu Waziri wa Barabara na Maendeleo ya Miji na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bandari na Bahari la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, akizungumza katika kongamano la Uchumi wa Bahari, aligusia suhula bora za Shirika la Bandari na Bahari katika nyanja ya usafirishaji.

Amesema suhula hizi zimewafanya wanaharakati wa ndani wa sekta binafsi, wawekezaji, wafanyabiashara na makampuni ya kigeni wawe na imani kuhusu Shirika la Bandari na Bahari la Iran.

Kwa kweli, maeneo ya bahari, kama yaliivyo maeneo ya nchi kavu, yana umuhimu maalumu katika kubadilishana bidhaa, na leo, nchi kama Iran ambazo zina pwani ndefu, pamoja na kuwa na umuhimu wa kimkakati, zina jukumu muhimu katika kuimarisha mabadilishano ya kibiashara. Mipaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na maji ya kimataifa inatambuliwa kuwa fursa ya kipekee katika mabadilishano ya kiuchumi ya Iran.

Bandar ya Chabahar ya Iran

Kuhusiana na hilo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamaenei ameitaja bahari kuwa ni medani ya makabiliano yenye nguvu na maadui, na wakati huo huo medani ya ufanisi na ushirikiano na marafiki. Pia mesisitiza umuhimu wa kupewa umuhimu sekta hiyo ya bahari. Kiongozi Muadhamu aidha ameashiria pwani ya Iran yenye urefu wa kilomita 2700 na kusema eneo hilo la habari lina utajiiri mkubwa na hivyo jitihada zote zinapaswa kufanyika ili kukuza sekta ya bahari na kutayarisha mazingiira mazuri kwa ajili ya nchi nyingine ambazo hazina bahari kama Afghanistan na nchi za Asia ya Kati.

Sekta ya bahari inapaswa kutiliwa maanani zaidi kutokana na ukweli kwamba, zaidi ya asilimia 90 ya mabadilishano ya kibiashara duniani yanafanywa kupitia njia za baharini. Kutokana na maendeleo muhimu katika miongo ya hivi karibuni, Iran ambayo ina mwambao mrefu katika Ghuba ya Uajemi, Bahari ya Oman na Bahari ya Kaspi, inaweza kuwa nchi yenye ushawishi zaidi katika sekta hii. Nukta hii inapata umuhimu hasa kwa kuzingatia kwamba Lango Bahari la Hormuz katika Ghuba ya Uajemi ni mojawapo ya njia kuu ya usafirishaji wa nishati ya mafuta na uagizaji wa bidhaa kwa nchi jirani na za kanda.

Tags