Iran yakadhibisha madai ya US ya kuipa silaha Yemen
(last modified Tue, 20 Feb 2024 12:53:28 GMT )
Feb 20, 2024 12:53 UTC
  • Iran yakadhibisha madai ya US ya kuipa silaha Yemen

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha vikali madai kwamba inatuma silaha nchini Yemen na kusisitiza kuwa, madai hayo hayana msingi wowote.

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Amir Saeid Iravani ameliandikia barua Baraza la Usalama la umoja huo akipinga madai hayo ya Washigton na kusisitiza kuwa hayana msingi.

Katika barua hiyo, Iravani amesema: Iran inaendelea kufungamana na maazimio nambari 2140 (2014) na 2216 (2015), na haijachukua hatua yoyote inayokwenda kinyume na maazimio hayo, ikiwemo kupeleka silaha Yemen.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameikosoa vikali Marekani kwa kuwasilisha habari za urongo kwa Baraza la Usalama na kutoa madai yasiyo na mashiko dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu juu ya kadhia ya Yemen na mzozo katika Bahari Nyeknundu.

Kuhusiana na mapigano katika Bahari ya Sham na mashambulizi yanayofanywa dhidi ya meli zinazoiunga mkono Israel, Iravani amesema, sababu ya hatua hiyo ni kuendelea hujuma za utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza na akasisitiza kuwa, usitishaji vita wa kudumu unapaswa kutekelezwa huko Gaza, ambao utakuwa thabiti na jumuishi; na uchokozi na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Israel lazima yakomeshwe pia.

Vikosi vya Yemen vimeendelea kufanya operesheni dhidi ya meli za US na UK katika Bahari Nyekundu

Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema: Jinai hizo za kinyama ni mfano wa wazi wa vitendo vya kibaguzi vya utawala ghasibu wa Israel ambavyo vinazidisha mateso ya wananchi wa Palestina na kuharibu misingi ya kurejeshwa amani ya kiadilifu na endelevu katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Iravani amezungumzia pia uungaji mkono wa Iran kwa mhimili wa muqawama na akasema: Uhusiano wa Iran na makundi ya muqawama ni aina ya mkataba wa kiulinzi kati ya makundi ya muqawama na Iran; na kwamba makundi hayo yanafanya maamuzi na  machaguo yao wenyewe na kuzingatia matashi na maslahi yao, lakini kwa ujumla yanafanya hivyo kwa uratibu na ushirikiano baina yao.

Iravani amesisitiza kuwa, "Kwa kuibua madai yasiyo na msingi, Marekani kwa mara nyingine tena amelitumia vibaya jukwaa la Baraza la Usalama kufuatilia ajenda yake ya kisiasa isiyo na maono ya mbali.

 

 

Tags