Haj Ali Akbari: Uchaguzi ni fursa nzuri kwa watu wa Iran
Imamu wa muda wa Swala ya Ijumaa iliyosaliwa leo hapa mjini Tehran amesema kuwa, uchaguzi ni fursa nzuri kwa watu wa Iran.
Hujjatul-Islam wal-Muslimin Mohammad Javad Haj Ali Akbari amesema hayo leo mbele ya hadhara ya waumini waliohudhuria ibada ya Swala ya Ijumaa mjini Tehran na kusisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa wiki ijayo.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran amebainisha kwamba, uchaguzi ni nembo ya uhuru na mfumo wa kidini nchini Iran wenye ridhaa ya wananchi.
Uchaguzi wa 12 wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran na uchaguzi wa sita wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu utafanyika tarehe Mosi ya mwezi ujao wa Machi.
Sheikh Haj Ali Akbari ameashiria pia kadhia ya kwanza ya ulimwengu wa Kiislamu na kimataifa yaani Gaza na kuibainisha kwamba, baada ya siku 140, vita vya Gaza vimekuwa dhihirisho kubwa la kushindwa kwa njia tofauti ubeberu wa kimataifa. Amesema, utawala ghasibu wa Israel umepata pigo kubwa kutoka kwa wanamapambano wa muqawama na kwa msaada wa Mungu na juhudi za muqawama sambamba na mwamko wa kimataifa uliotokea, utawala huu katu hautaona siku nzuri.
Kadhalika khatibu wa Swala ya Ijumaa amesema, mauaji na uharibifu wa miundo mbinu huko Palestina na Gaza ni zao la demokrasia ya kiliberalio ya nchi za Magharibi na kimya cha usaliti wa baadhi ya serikali zinazojiita za Kiislamu.