Iran yaionya UN: Marekani inashadidisha taharuki katika eneo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali juhudi za Marekani za kushadidisha hali ya taharuki katika Bahari Nyekundu na Yemen na kuonya kuwa, hatua hizo za kijeshi za Washington hazitakuwa na matokeo mengine isipokuwa kuvuruga jitihada za pamoja za Iran na Umoja wa Mataifa katika eneo la Asia Magharibi.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim; Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian ametoa indhari hiyo katika mazungumzo yake na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres huko mjini Geneva, Uswisi pambizoni mwa kikao cha 55 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC).
Amesema Marekani haina azma ya kusaidia kusimamisha vita dhidi ya Ukanda wa Gaza, ambako utawala wa Kizayuni umeua kwa umati maelfu ya Wapalestina wa eneo hilo, huku ukitaka kuwaua waliosalia kwa njaa.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesema Umoja wa Mataifa lazima uzitake nchi zote wanachama kuacha kushirikiana na utawala wa kibaguzi wa Israel katika kutenda jinai kubwa zaidi za kimataifa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres sanjari na kuishukuru Iran kwa juhudi zake za kidiplomasia za kujaribu kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Palestina kwa njia za kisiasa, amekosoa vikali 'adhabu jumla' dhidi ya Wapalestina.
Kadhalika jana Jumatatu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliuambia mkutano wa 55 wa ngazi ya mawaziri wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC) kwamba, kutochukua hatua za maana Baraza la Usalama la umoja kuzuia mauaji ya kimbari ya Wapalestina wa Gaza ni janga la kidiplomasia.
Amir-Abdollahian ameonya kuhusu mauaji ya umati yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wakazi wa Rafah huko Palestina na kusisitiza kuwa, dunia ina wajibu wa kuibebesha dhima Ikulu ya Marekani ya White House.
Amesema: Iran inaamini kuwa, kutuma silaha ili mauaji ya kimbari ya Wapalestina yaendelee ni kosa lisilosameheka, na kukata ushirikiano hasa wa kiuchumi na kibiashara na utawala wa apartheid wa Israel ndiyo hatua ya dharura inayopasa kuchukuliwa na serikali na nchi zote za dunia.