Waziri: Uzalishaji wa gesi ya Iran umeongezeka licha ya vikwazo
Waziri wa Mafuta wa Iran amesema uzalishaji wa gesi ya Jamhuri ya Kiislamu umeendelea kuongezeka siku baada ya siku, licha ya vikwazo vya Wamagharibi dhidi ya sekta ya nishati ya taifa hili.
Javad Owji amesema hayo Jumamosi pambizoni mwa Mkutano wa Saba wa Wakuu wa Nchi Zinazouza Gesi Kwa Wingi Duniani (GECF) huko Algiers, mji mkuu wa Algeria.
"Takwimu za punde za kimataifa zimethiibitisha uhalisia kwamba, uzalishaji wa gesi ya Iran upo katika mkondo wa kukwekea tokea mwaka 2011, na vikwazo batili na haramu vya Marekani vimeshindwa kusimamisha ongezeko hilo," amesema Waziri Owji.
Ameeleza bayana kuwa, uzalishaji wa gesi ghafi umeongezeka kwa asilimia 5.2 kwa mwaka, baina ya mwaka 2012-2022. Owji amefafanua kuwa, kiwango hicho ni mara 2.5 zaidi ya kiwango cha wastani cha uzalishaji wa gesi dunia katika muda huo.
Waziri wa Mafuta wa Iran amebainisha kuwa, licha ya changamoto za hapa na pale katika soko la gesi duniani, lakini Jumuiya ya Nchi Zinazouza Gesi Kwa Wingi Duniani (GECF) zimejitahidi katika kuimarisha ushirikiano wao, na kuandaa stratajia ya muda mrefu ya kukabili changamoto hizo.
GECF ina nchi 14 wanachama na viongozi 11 wa jumuiya hiyo akiwemo Rais Seyed Ebrahim Raisi wa Iran wanashiriki kikao cha leo Jumamosi jijini Algiers cha kujadili mustakabali wa sekta hiyo.
Waziri wa Mafuta wa Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu sasa inajitosheleza kikamilifu katika sekta ya uchimbaji mafuta na gesi, baharini na katika nchi kavu na kwamba hivi sasa Iran inajitosheleza kikamilifu katika sekta zote zinazohusiana na mafuta na gesi na haihitajii chochote kutoka nje ya nchi katika kazi zake hizo.