Iran yaipongeza Afrika Kusini kwa kuishtaki Israel katika mahakama ya ICJ
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameipongeza na kuishukuru Afrika Kusini kwa uamuzi wake wa kihistoria wa kuwasilisha kesi dhidi ya utawala haramu wa Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), kuhusu jinai za mauaji ya kimbari zinazotekelezwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
Ensiyeh Khazali, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia masuala ya wanawake na familia amenukuliwa na shirika la habari la IRNA akisema kuwa Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono uamuzi huo wa busara wa Pretoria, wakati wa mazungumzo yake na Lindiwe Zulu, Waziri wa Ustawi wa Jamii wa Afrika Kusini pambizoni mwa Kikao cha 68 cha Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Nafasi ya Mwanamke mjini New York.
Khazali ametoa mwito kwa nchi zote za dunia kuchukua hatua za kivitendo za kuunga mkono hatua ya Afrika Kusini ya kuuburuza utawala wa Kizayuni katika mahakama ya ICJ, ili kukomesha janga la kibinadamu linaloshuhudiwa Gaza.
Utawala haramu wa Israel umedharau uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki wa kuutaka uchukue hatua zote zinazohitajika kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, na badala yake jeshi la utawala huo pandikizi limeendelea kumwaga damu za Wapalestina wa Gaza.
Kadhalika Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria uhusiano mzuri na uliokita mizizi baina ya Jamhuri ya Kiislamu na Afrika Kusini na kusisitiza kuwa, hakuna kikwazo chochote cha kuzuia kuimarishwa zaidi uhusiano huo wa pande mbili.
Khazali ameeleza kuwa, baada ya kusainiwa hati za maelewano baina ya Iran na Afrika Kusini, kuna haja ya kuchukuliwa hatua za kivitendo ili kuharakisha mchakato wa kuimarisha hali za wanawake na kupiga jeki ushirikiano wa pande mbili katika nyuga za uchumi, elimu ya sanaa na familia pamoja na nafasi za ajira za kidijitali.
Kwa upande wake, Lindiwe Zulu, Waziri wa Ustawi wa Jamii wa Afrika Kusini huku akitoa mwito wa kuwepo amani kote duniani, amesisitiza kuwa nchi yake itaendelea kuwaunga mkono wananchi wa Palestina hasa wakazi wa Gaza.