Apr 13, 2024 11:57 UTC
  • Kuwa jadi Iran katika kujibu shambulio na kuongezeka harakati na mashauriano ya Wamagharibi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amejibu simu alizopigiwa na Annalena Baerbock, David Cameron na Penny Wong Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Uingereza na Australia.

Katika mazungumzo hayo ya simu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: Wakati utawala wa Kizayuni unapokiuka kinga ya watu binafsi na maeneo ya kidiplomasia kwa mujibu wa sheria za kimataifa na Mikataba ya Vienna, huku Baraza la Usalama likinyamaza kimya na kushindwa kutoa tamko la kulaani shambulio la kigaidi dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus, ni jambo la dharura kujihami kisheria na kuuadhibu upande chokozi. 

Hossein Amir Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza kuwa Iran haitaki kupanua vita lakini usalama thabiti katika eneo nyeti la Asia Magharibi unahusiana na kuwazuia viongozi wa utawala wa Kizayuni wapenda vita na kusimamisha kikamilifu jinai za kivita za utawala huo dhidi ya Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.  

Hossein Amir Abdollahian 

Wakati huo huo, dunia  inajitayarisha kushuhudia jibu la Iran kufuatia shambulio la utawala wa Kizayuni katika jengo la ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus Syria na kuuliwa shahidi washauri wa Iran huku Wazayuni wakiwa wamekumbwa na hofu na wasiwasi na nchi za Magharibi zikifanya mashauriano ili kuizuia Iran kulipiza kisasi. Kama walivyoeleza maafisa wa ngazi za juu wa Iran, kipigo kwa Israel ni jambo lisilo na shaka na tayari uamuzi wa mwisho kuhusu namna ya kuujibu utawala wa Kizayuni umeshachukuliwa. Viongozi wa utawala wa Kizayuni wanahofia kwamba hatua ya kulipiza kisasi itakuwa na uhalali kamili wa kisheria kwa mujibu  mtazamo wa sheria na kanuni za kimataifa. 

Shambulio dhidi ya maeneo ya kidiplomasia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Vienna wa 1961 wa Mahusiano ya Kidiplomasia, na pia ukiukaji wa wazi wa sheria za Mkataba wa Mwaka 1973 wa Kuzuia Uhalifu dhidi ya Shakhsia wa Kimataifa ikiwa ni pamoja na wanadiplomasia. Mikataba hii tajwa inaeleza kuwa ni marufuku kutekeleza shambulio lolote la kikatili dhidi ya maeneo rasmi na makazi ya watu wa taasisi za kimataifa, pamoja na wanadiplomasia.

Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran walianzisha hatua za kidiplomasia mara tu baada ya utawala wa Israel kuushambulia ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran huko Damascus na hivyo kukiuka wazi wazi sheria za kimataifa. Katika mkondo huo, Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja jwa Mataifa alimuandikia barua Katibu Mkuu wa UN na Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la umoja huo na kuitaka taasisi hiyo kulaani shambulio la Israel na kuchukua uamuzi unaofaa katika uwanja huo. Kufuatia hilo, Russia pia iliitaka Malta ambayo inashikilia uwenyekiti wa kiduru wa Baraza la Usalama mwezi huu wa Aprili iitishe kikao cha wazi cha baraza hilo. 

Hujuma ya Israel katika ubalozi mdogo wa Iran Syria 

Mkutano huo ulifanyika tarehe Pili Aprili mwaka huu, ambapo wawakilishi wa nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa walilaani shambulio la utawala wa Israel dhidi ya ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Damascus, katika kikao cha dharura cha baraza hilo na kutahadharisha kuhusu hatua za utawala huo na machafuko zaidi katika eneo. Hata hivyo nchi tatu yaani Marekani, Uingereza na Ufaransa na pia waitifaki wa nchi hizo  yaani Korea Kusini na Japan si tu hazijalaani shambulio hilo la Israel bali zimezuia kuwasilishwa azimio la Baraza la Usalama la kulaani hujuma hiyo.   

Lau Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lingelaani hujuma ya utawala wa Kizayuni ya kushambulia maeneo ya kidiplomasia ya Iran huko Damascus, na baadaye kuwafungulia mashitaka wahusika wake, pengine Iran isingekuwa na haja na ulazima wa kuuadhibu utawala huo. Hii ni katika hali ambayo kwa mujibu wa Kifungu cha 24 cha Mkataba huo wa Vienna, Baraza la Usalama, kwa niaba ya wanachama wote wa Umoja wa Mataifa lina wajibu na jukumu kuu la kulinda amani na usalama wa dunia, hata hivyo baraza hilo halijawahi kutekeleza majukumu na wajibu wake ulioainishwa katika kesi zinazoihusu Israel; na hii imekuwa moja ya sababu kuu za kuchukua muda mrefu mgogoro wa Palestina na Mashariki ya Kati katika miongo minane iliyopita.