Apr 18, 2024 02:33 UTC
  • Vikwazo vipya vya Marekani; muendelezo wa sera iliyofeli dhidi ya Iran

Kufuatia kushindwa utawala wa Kizayuni na Marekani katika kukabiliana na mashambulizi ya kulipiza kisasi ya ndege zisizo na rubani na makombora ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel), Washington kwa mara nyingine inajaribu kuiwekea Iran vikwazo vipya vya silaha.

Mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani Jack Sullivan amesema: Washington itaweka vikwazo vipya dhidi ya Iran katika siku zijazo. Vikwazo hivi vitalenga mpango wa makombora na ndege zisizo na rubani pamoja na mashirika na taasisi zinazounga mkono Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Wizara ya Ulinzi. Marekani inatarajia kuwa washirika wake wataiunga mkono katika vikwazo vyake dhidi ya Iran.
Hatua hii ya Marekani inafanyika baada ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kutekeleza operesheni kubwa ya kulipiza kisasi mapema Jumapili ambapo ilivurumisha ndege zisizo na rubani, makombora ya balistiki na ya cruise kwa mafanikio kueleketa  ngome za kijeshi za utawala wa Kizayuni wa Israel. Katika operesheni hiyo, makombora ya IRGC yalilenga kwa mafanikio kituo cha ndege za kivita cha Navatim ambacho kinahifadhi ndege za kivita za kisasa za F-35 za kikosi cha anga cha Jeshi la Israel. Operesheni hiyo iliyopewa jina la  'Ahadi ya Kweli' na ambayo ilifanyika kwa msingi wa Ibara ya 51 ya Hati ya Umoja wa Mataifa, ilikuwa ni jibu la shambulio la anga la utawala wa Israel Aprili Mosi dhidi ya jengo la ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Damascus, ambapo makamanda na washauri 7 wa kijeshi wa IRGC waliuawa shahidi.
Licha ya msaada mkubwa wa kiufundi, zana za kivita na kijasusi uliotolewa na Marekani kwa utawala wa Kizayuni, mfumo wa ulinzi wa utawala huo ujulikanao kama 'Kuba la Chuma' ulishindwa kuzuia mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani za Iran, na hivi sasa Wamagharibi wakiongozwa na Marekani, wameamua kuwa njia bora zaidi ya kujibu mapigo ni kuiwekea Iran vikwazo vipya ambavyo vinalenga mpango wa Iran wa kujihami wa makombora na ndege zisizo na rubani.

Ni dhahiri kwamba vikwazo hivyo vipya vyote vina  maana ya kukiri kushindwa kijeshi Marekani na utawala wa Kizayuni mkabala wa Iran. Hali kadhalika vikwazo hivyo vipya ni dalili ya kushindwa vikwazo vya zamani ambavyo vilikuwa na lengo la kuzuia ukuaji na maendeleo ya viwanda vya silaha vya Iran zikiwemo sekta za makombora na ndege zisizo na rubani.

Kombora la Emad la Iran

Maendeleo ya Iran katika uga wa makombora na ndege zisizo na rubani yamepatikana katika kipindi hiki cha vikwazo.
Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani iliiwekea vikwazo vikubwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na kwa mujibu wa Idara ya Utafiti ya Congress (CRS), vikwazo hivi vinapiga marufuku takriban biashara zote za Marekani na Iran, kuzuia mali za serikali ya Iran Marekani na kuzuia misaada ya kigeni na mauzo ya silaha kwa Iran. Tarehe 18 Oktoba 2023, wakati wa kumalizika muda wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya mradi wa makombora wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Idara ya Fedha ya Marekani ilitangaza kuwekewa vikwazo vipya mpango wa Iran wa makombora ya balistiki na ndege zisizo na rubani.
Kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kizuizi cha miaka minane cha baraza hilo dhidi ya shughuli za makombora ya Iran, pamoja na usambazaji, uuzaji  wa vifaa na teknolojia zinazohusiana na maendeleo ya uwezo wa makombora ya Iran, ulimalizika tarehe 27 Oktoba 2019.

Kwa hivyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kama nchi nyingine yoyote, ina haki ya kuchagua njia zake za ulinzi kwa kuzingatia sheria za kimataifa. Kuimarisha uwezo wa makombora na ndege zisizo na rubani za Iran pia kunalenga kukidhi mahitaji halali ya kiulinzi kwa mujibu wa Kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa.
Kuhusiana na suala hilo, vikosi vya jeshi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimeazimia kufuatilia uimarishaji wa uwezo wa silaha, na kuzidisha maendeleo ya Iran katika uga wa utengenezaji wa makombora ya balistiki na cruise pamoja na uundaji wa aina mbali mbali za ndege zisizo na rubani. Matokeo ya azma hii ni kushindwa adui katika kukabiliana na mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran hivi karibuni.