Apr 18, 2024 04:42 UTC
  • Iran yapinga hukumu ya mahakama ya Argentina kuhusu mashambulizi ya mabomu

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kanani, ametupilia mbali uamuzi wa mahakama ya Argentina unaoilaumu Iran kwa mashambulizi mawili ya mabomu nchini humo katika muongo wa 90, na kuyataja madai katika hukumu hiyo kuwa yasiyo na ushahidi na yenye msukumo wa kisiasa.

Katika taarifa ya Jumatano, Kanani alikuwa akiashiria uamuzi wa hivi majuzi wa Mahakama ya Cassation ya Argentina, ambayo ilihusisha Iran na harakati ya Hizbullah  ya Lebanon na mashambulizi mawili dhidi ya ubalozi wa Israel na Kituo cha Kiyahudi cha Argentina (AMIA) huko Buenos Aires.

Uamuzi huo, kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari, ulidai kwamba Iran ilipanga shambulio la 1992 kwenye ubalozi wa Israeli na shambulio la 1994 katika kituo cha AMIA.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran  amesema kesi hiyo inadhihirisha utekelezaji wa mradi mpya wa kisiasa unaofanywa na mahasimu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hususan utawala wa Kizayuni.

Msemaji huyo amesisitiza kuwa katika kipindi cha miaka thelathini iliyopita, Iran imekuwa ikiunga mkono jitihada sahihi za kubaini ukweli wa tukio hilo, ikiwa ni pamoja na kutia saini mkataba wa maelewano na serikali ya Argentina ili kuunda tume ya pamoja ya uchunguzi. Amesema kwa bahati mbaya, jitihada za utatuzi hazijazaa matunda  kutokana na hitilafu za kisiasa ndani ya Argentina.

Kanani ametahadharisha kuwa utawala wa Israel unajaribu mara kwa mara kubadili muelekeo kutoka kwenye mauaji ya kimbari huko Gaza, akisisitiza kwamba huenda njama hizo za Israel zimeathiri uamuzi wa hivi karibuni wa mahakama hiyo ya Argentina.