Apr 19, 2024 02:46 UTC
  • Iran yalaani madai ya viongozi wa Ulaya na mawaziri wa fedha wa G7 dhidi yake

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekanusha madai ya viongozi wa nchi za Ulaya na mawaziri wa fedha wa kundi la G7 pamoja na matamshi ya baadhi ya wakuu wa Marekani na kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitosita hata mara moja kujihami na kulinda maslahi yake ya kitaifa.

Shirika la habari la FARS limemnukuu Nasser Kan'ani akisema hayo jana Alkhamisi kujibu madai yaliyomo kwenye tamko la hivi karibuni la viongozi wa Ulaya na mawaziri wa fedha wa kundi la G7 pamoja na baadhi ya viongozi wa Marekani na kusema kuwa, misimamo kama hiyo ya kinafiki ilitarajiwa tangu zamani kuchukuliwa na pande hizo na haikubaliki kabisa.

Kundi la G7

 

Wakuu wa kundi la G7 linaloundwa na Ufaransa, Marekani, Uingereza, Ujerumani, Japan, Italia na Canada wametoa taarifa ya pamoja ya kulaani shambulio la kulipiza kisasi na la kumtia adabu adui Mzayuni lililofanywa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya utawala pandikizi wa Israel kushambulia ubalozi wa Iran mjini Damascus Syria.

Kan'ani amesema, inasikitisha kuona kuwa madola yanayojifanya ni viraja wa kupigania haki za binadamu na kuheshimu sheria za kimtaifa yalichukua msimamo wa kindumilakuwili baada ya utawala wa Kizayuni kushambulia ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus Syria na sasa hivi madola hayo hayo yamejitokeza kifua mbele kulaani majibu yaliyotolewa na Jamhuri ya Kiislamu licha ya kwamba majibu hayo yametolewa kwa kuchunga kikamilifu sheria zote za kimataifa na hakuna nchi yoyote inayoweza kuvumilia kushambuliwa ubalozi wake.

Vilevile ameelezea wasiwasi wake juu ya jinsi nchi kama Marekani na za Ulaya zinavyohatarisha amani, utulivu na usalama wa eneo la Asia Magharibi katika kipindi cha nusu nzima ya karne iliyopita na kulaani jinsi madola hayo ya kibeberu yalivyoupandisha kiburi utawala wa Kizayuni na kujiona uko juu ya sheria zote za kimataifa.