Apr 22, 2024 12:18 UTC
  • Iran: Operesheni ya Ahadi ya Kweli imeonesha uratibu bora wa kidiplomasia na kijeshi nchini

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, uratibu baina ya chombo cha demokrasia na Komandi Kuu ya Vikosi vya Ulinzi vya Iran katika kutekeleza operesheni ya kuitia adabu Israel iliyopewa jina la "Operesheni ya Ahadi ya Kweli" umekuwa na matunda mazuri sana kwa Iran, kimataifa.

Tarehe Mosi Aprili 2024, utawala wa Kizayuni ulifanya jinai ya kushambulia kigaidi ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus Syria na kuua shahidi washauri 7 wa ngazi za juu wa kijeshi wa Iran..

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ambaye pia ndiye Amirijeshi Mkuu wa majeshi yote ya Iran alitangaza wazi kuwa, hatua ya Tel Aviv ya kushambulia ubalozi wa Iran huko Damascus ni sawa na kushambulia ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu na hivyo lazima Israel itashikishwa adabu.

Ndio maana usiku wa kuamkia Jumapili ya tarehe 14 mwezi huu wa Aprili, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran (SEPAH) liliendesha operesheni ya "Ahadi ya Kweli"  kwa kuyatwanga kwa makombora na droni maeneo mbalimbali ya utawala wa Kizayuni na kumtia adabu adui Mzayuni. 

Leo Jumatatu, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Nasser Kan'ani Chafi amesema kuwa, uratibu mzuri uliooneshwa baina ya chombo cha demokrasia na Komandi Kuu ya Vikosi vya Ulinzi vya Iran katika kutekeleza operesheni hiyo ya Ahadi ya Kweli umekuwa na matunda mazuri sana kwa Iran, kimataifa.

Aidha amesema, Marekani ni sehemu ya mgogoro wa Ghaza tangu utawala wa Kizayuni ulipoanzisha mashambulizi ya kikatili kwenye ukanda huo na kuongeza kuwa, misaada ya kifedha ya Marekani kwa utawala wa Kizayuni ni sehemu ya kuutunza na kuupongeza utawala huo kwa jinai zake dhidi ya Wapalestina.