May 09, 2024 03:36 UTC
  • Magharibi iliiomba Iran 'isiipige sana Israel', ipunguze ukali wa operesheni ya Ahadi ya  Kweli

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema nchi za Magharibi ziliiomba Jamhuri ya Kiislamu ijizuie na ipunguze ukali wa operesheni yake ya kulipiza kisasi dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, kabla ya kushambulia vituo vya utawala huo mwezi uliopita kujibu mapigo kwa shambulio lake la kigaidi ulilofanya dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria.

Hossein Amir-Abdollahian amesema, "kabla ya operesheni, ombi la Wamagharibi lilikuwa ni kwamba ikiwa mumeamua kujibu mapigo, msipige sana na punguzeni ukali wa operesheni".
 
 Amir-Abdollahian alitoa kauli hiyo mbele ya waandishi wa habari jana Jumatano pembeni ya kikao cha kila wiki cha Baraza la Mawaziri.
 
Katika shambulio mchanganyiko lililopewa jina la Operesheni Ahadi ya Kweli, jeshi la Iran lilirusha makombora na ndege zisizo na rubani zaidi ya 300 kupiga vituo na maeneo ya utawala wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel usiku wa Aprili 13 kujibu jinai iliyofanywa na utawala huo Aprili Mosi dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran katika mji mkuu wa Syria, Damascus. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa, tangu ilipoamuliwa kutekelezwa Operesheni Ahadi ya Kweli, Wamagharibi na washirika wa Marekani barani Ulaya walianzisha mawasiliano makubwa na Iran, na ombi lao la kwanza lilikuwa ni kuitaka Iran ijizuie na isijibu mapigo, lakini Jamhuri ya Kiislamu ikasisitiza kwamba lazima itachukua hatua dhidi ya Israel kwa wakati itakaoamua na kwa namna itakavyoona inafaa bila kuathiriwa na mashinikizo ya yeyote.

Amir-Abdollahian ameongeza kuwa, pamoja na hayo Jamhuri ya Kiislamu iliueleza upande wa Magharibi na Marekani kwamba mzizi wa tatizo hasa ni mgogoro wa Ghaza ambao unapaswa kutatuliwa na wao Wamagharibi inawapasa walizingatie suala hilo.
 
Aidha amesema, "tulikuwa na makubaliano yasiyo ya maandishi na pande za Magharibi ya kuzingatia usitishaji vita huko Ghaza, na wao Wamagharibi walisema watachukua hatua katika muelekeo huo; na leo, dalili chanya zimeonekana katika suala hili".../ 

 

Tags