Rouhani: Ikilazimu, Iran itarejea katika mpango wa awali wa nyuklia
Rais Hassan Rouhani wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuheshimu na kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya Vienna, lakini ameonya kuwa Tehran haitasita kutoa jibu iwapo upande wa pili utakosa kutekeleza makubaliano hayo ipasavyo.
Akiongea mjini Tehran hii leo katika hafla ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu kufikiwa kwa makubaliano hayo, Rais Rouhani amesema Jamhuri ya Kiislamu haitachelea kurejesha miradi yake ya nyuklia katika kiwango itakacho iwapo upande wa pili hautatekeleza wajibu wake ipasavyo.
Rais Rouhani amesema kuwa: "Kutekelezwa makubaliano hayo yanayojulikana kama Utekelezaji wa Mpango wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA kuna maslahi kwa pande zote katika masuala ya usalama, amani maendeleo na uthabiti wa nchi zote za dunia na iwapo yatakosa kutekelezwa, basi itakuwa hasara kwa kila mmoja."
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema yeyote akayekiuka makubaliano hayo, basi atapata hasara kubwa isiyopimika katika uga wa kimataifa.
Makubaliano hayo ya nyuklia yaliyofikiwa Julai 14 mwaka jana mjini Vienna nchini Austria kati ya Iran na Kundi la 5+1, licha ya kuanza kutekelezwa Januari mwaka huu, lakini Tehran imekuwa ikilalamikia mwendo wa kinyonga wa utekelezaji wake.