May 26, 2024 10:46 UTC
  • Mokhber: Mkakati wa Iran wa kuunga mkono Muqawama hautabadilika baada ya kufa shahidi Sayyid Raisi

Rais wa muda wa Iran amesema stratejia kuu ya Jamhuri ya Kiislamu katika kutoa msukumo na uungaji mkono kwa vuguvugu la Muqawama hususan kwa makundi ya Muqawama ya Palestina haitabadilika kwa sababu ya mabadiliko ya watu.

Mohammed Mokhber, Rais wa muda wa Iran ametoa sisitizo hilo katika mazungumzo ya simu aliyofanya na Ziyad al-Nakhalah, Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina-, ambapo sambamba na kuushukuru Muqawama wa Palestina kwa kuungana na Serikali pamoja na wananchi wa Iran katika msiba mkubwa wa kuondokewa na Rais na maafisa alioandamana nao waliokufa shahidi katika ajali ya helikopta- amebainisha kuwa, mkakati wa Muqawama ndiyo njia mwafaka na athirifu zaidi ya kukabiliana na jinai na hujuma za utawala wa Kizayuni wa Israel unaofanya mauaji ya kimbari na akaongeza kuwa, operesheni ya "Ahadi ya Kweli" ni moja ya matokeo ya harakati ya Muqawama, ambayo iliporomosha haiba ya Marekani na utawala bandia wa Israel.
Ziyad Al-Nakhalah

Kwa upande wake, Ziyad Al-Nakhalah ametoa mkono wa pole kwa Serikali na wananchi wa Iran kwa tukio la kufa shahidi Rais Sayyid Ebrahim Raisi na Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian, pamoja na maafisa wengine waliokufa shahidi pamoja nao na kueleza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaushinda na kuuvuka msukosuko huu kutokana na kubarikiwa kuwa na Kiongozi mkubwa, maafisa wenye uwezo unaostahiki na wananchi wenye mawazo na fikra za kimapinduzi.

 
Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul-Islami ya Palestina vilevile ameeleza kuwa, Shahidi Raisi na Shahidi Amir-Abdollahian daima walikuwa mstari wa mbele katika kutetea manufaa na maslahi ya taifa la Iran na kuunga mkono Vuguvugu la Muqawama, na akamueleza Rais wa muda wa Iran kuwa ni shakhsia mwenye uwezo unaotakikana wa kujaza pengo lililoachwa kutokana na msiba huu mkubwa wa kuondokewa.

Helikopta iliyokuwa imembeba Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Jumapili jioni Mei 19, 2024 ilipata ajali ilipokuwa ikirejea kutoka kwenye hafla ya ufunguzi wa bwawa la Qiz Qalasi kwenye mpaka wa pamoja wa Iran na Jamhuri ya Azerbaijan.

Wakati helikopta hiyo ilipokuwa inaelekea mji wa Tabriz, ilianguka katika eneo la Varzghan mkoani Azarbaijan Mashariki, kaskazini-magharibi mwa Iran. Ndani yake walikuwemo pia Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje, Imam wa Ijumaa wa Tabriz, Gavana wa Azarbaijan Mashariki na watu wengine; na wote pamoja wakaifika hadhi tukufu ya kufa shahidi.../