Jun 26, 2024 09:18 UTC
  • Ushiriki wa kiwango cha juu zaidi; mkakati wa kudumu wa Kiongozi wa Mapinduzi kuhusu uchaguzi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria uchaguzi muhimu sana wa siku ya Ijumaa (28 Juni), na kusisitizia ushiriki wa kiwango cha juu kabisa wa wananchi na kuwataka wananchi wa taifa hili kujitokeza katika vituo vya kupigia kura Ijumaa ya keshokutwa ili kumchagua Rais mpya.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, alisema hayo jana (Jumanne Juni 25) alipokutana na maelfu ya wananchi katika sherehe ya maadhimisho ya Sikukuu ya Eid Ghadir Khum hapa mjini Tehran na kusisitiza kwamba, ushiriki mkubwa na wenye hamasa wa taifa katika uchaguzi ujao wa rais, kuwa ni dhihirisho la nguvu ya kitaifa, dhamana ya usalama wa taifa na jambo linalowakatisha tamaa maadui wa Iran.

Wairani waliiotimiza masharti ya kupiga kura Ijumaa ya keshokutwa wanatazamiwa kushiriki kwa wingi katika uchaguzi wa 14 wa Rais wa Iran, kumtafuta atakayejaza nafasi iliyoachwa wazi na Rais Ebrahim Raisi, ambaye alikufa shahidi katika ajali ya helikopta akiwa na maafisa wengine mnamo Mei 19 akiwemo Waziri wa Mashauri ya Kigeni Hussein Amir Abdollahian.

Sasa ni wakati wa watu kuchagua. Moja ya stratijia muhimu ambayo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu daima amekuwa akiitilia mkazo kuhusu uchaguzi, ni kuandaliwa mazingira ya wananchi kuwa na ushiriki wa kiwango cha juu zaidi. Katika suala hili, ni muhimu kutaja nukta kadhaa ambazo ni muhimu.

 

Mosi; sisitizo la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi juu ya ulazima wa ushiriki wa juu zaidi wa wananchi katika uchaguzi huo ni kubatilisha madai na shutuma zote zinazotolewa na wapinzani na maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu ushiriki katika uchaguzi huo.

Maadui wanatoa madai na kusema uwongo kwamba, eti Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haiandai mazingira ya kuweko ya wananchi kuwa na ushiriki mkubwa katika uchaguzi. Madai haya yanatolewa licha ya ukweli kwamba, wastani wa ushiriki katika uchaguzi wa rais wa Iran katika duru 13 zilizopita ni takriban 64%.

Wakati huo huo Ayatullah Khamenei alisisitiza katika hotuba yake ya jana kwamba: Jamhuri na kushirikishwa wananchi ndio asili ya Jamhuri ya Kiislamu ambayo kuchaguliwa na kuteuliwa mkuu wa nchi ndio dhihirisho lake muhimu zaidi.

Pili; katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ushiriki wa watu daima umefafanuliwa kuwa ni mojawapo ya misingi na nguzo muhimu za nguvu na mamlaka.

Uhusiano baina ya watu na mfumo wa kisiasa katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni uhusiano uliojengeka juu ya msingi wa nguvu na uthabiti wa pande zote. Kwa maana kwamba, watu kwa kuwa na mahudhurio ya kiwango cha juu zaidi wanaimarisha mfumo wa kisiasa, na mfumo wa kisiasa nao unaandaa mazingira ya kuleta usalama na ustawi zaidi. Suala hili lipo katika dira ya kisiasa ya Imam Khomeini (RA), mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiiislamu.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

 

Imam Khomeini alisema kuhusiana na hili: "Uhusiano kati ya nguzo za kiutendaji na za kiserikali ni kama mizani." Upande mmoja ni serikali, bunge na rais, na upande mwingine ni wananchi. Kwa hali yoyote, ni muhimu kudumisha pande hizi mbili ili mizani ibakie kuwa sawa na isiegemee upande mmoja, na hakuna kitu kinachoweza kufanywa bila ya himaya na uungaji mkono wa wananchi.

Katika hotuba yake ya jana, Ayatullah Khamenei alisisitiza nukta hii kwamba: Kila mwenye kupenda kuweko Iran yenye nguvu na ya fahari basi ashiriki katika uchaguzi. Akizungumzia kuendelea hasama na uadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu tangu ilipoasisiwa hadi hivi sasa, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, chaguzi na ushiriki mkubwa wa wananchi ni miongoni mwa sababu za kusambaratisha na kushinda uadui.

Nukta ya tatu;  umuhimu wa ushiriki wa watu na kuchaguliwa rais na wananchi ni muhimu katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kiasi kwamba, baada ya kifo, kuuzuliwa au kujiuzulu kwa rais, uchaguzi mpya lazima ufanyike ndani ya siku 50. Jambo hili pia linahesabiwa kuwa miongoni mwa mambo yanayodhihirisha uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kadhalika Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kufanyika uchaguzi, siku 40 tu baada ya kuaga dunia Rais mzuri wa nchi, mpendwa, mtu wa watu, mtendaji na mchapaka kazi na ambaye aliagwa na kusindikizwa na na mamilioni ya watu, ni jambo adimu  na nadra mno kushuhudiwa duniani.