May 30, 2024 05:52 UTC
  • Kupunguza umaskini na kuimarisha uchumi nchini ni urithi mwingine wa Shahid Rais Raisi

Ehsan Khanduzi, msemaji wa masuala ya kiuchumi wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia, kiwango cha umaskini nchini kimepungua kwa asilimia 7.4 kutoka asilimia 29.3 hadi 21.9.

Amesema hayo ni licha ya ukweli kwamba Benki ya Dunia na mashirika ya kimataifa ya kifedha hayana mtazamo wa huruma kwa watu wa Iran wala serikali ya Ayatollah Raisi, lakini kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi imekuwa kubwa kiasi kwamba imekuwa vigumu kupuuzwa na kufumbiwa macho na taasisi za kifedha kimataifa. Ukuaji wa uchumi wa mwaka huu na wa mwaka ujao ni zaidi ya ukuaji wa mwaka uliopita. Benki ya Dunia hivi karibuni ilichapisha takwimu kuhusu hali ya umaskini katika nchi tofauti za dunia, ikiwemo Iran. Shirika hili la kimataifa limewasilisha viashiria vitatu vya mistari ya umaskini, ambavyo ni pamoja na mstari wa umaskini uliokithiri wenye kipato cha kila siku cha dola 2.15 kwa mtu, mstari wa umaskini wenye kipato cha kila siku cha dola 3.65 na mstari wa umaskini wenye kipato cha kila siku cha dola 6.85 kwa mtu.

Uchunguzi wa takwimu za Benki ya Dunia kuhusu hali ya umaskini nchini Iran unaonyesha kuwa serikali ya 13 imepata mafanikio makubwa katika kupunguza umaskini nchini kwa kuzingatia mistari yote mitatu ya umaskini iliyoainishwa na benki hii. Idadi ya watu wanaokabiliwa na umaskini mkubwa nchini Iran, ambayo imefafanuliwa kwa mujibu wa mapato ya kila siku ya dola 2.15 kwa mtu mwanzoni mwa serikali ya 13, ilikuwa sawa na asilimia 0.8 ya idadi ya watu wote nchini, lakini takwimu hii ilipungua hadi asilimia 0.7 mwaka 2021 na hadi asilimia 0.5 mwaka 2022.

Kwa utaratibu huo, umaskini mkubwa nchini Iran umekuwa ukipungua kwa miaka miwili mfululizo ambapo idadi ya watu walio katika umaskini huo imekuwa ikipungua na kufikia kiwango cha chini zaidi katika miaka mitano iliyopita. Hali ya Iran katika kiashiria cha pili cha umaskini, yaani watu wenye kipato cha chini ya dola 3.65 kwa siku, pia imeimarika sana katika serikali ya 13. Kulingana na makadirio ya Benki ya Dunia, mnamo 2020, zaidi ya asilimia 6 ya watu wa Iran walikuwa na mapato ya kila siku ya chini ya dola 3.65, lakini takwimu hii ilipungua hadi asilimia 5 mnamo 2021 na hadi asilimia 4 mwaka 2022, ambacho ni kiwango cha chini kabisa tangu 2017. Takwimu za Benki ya Dunia pia zinaonyesha kuwa mwaka 2022, zaidi ya asilimia 22 ya wakazi wa Iran walikuwa na mapato ya kila siku ya dola 6.85.

Ajali ya helijopta iliyopelekea kufa shahidi Ayatullah Raisi na wenzake

Idadi hii ni chini ya asilimia 25 ambayo ilirekodiwa mwaka 2021. Mwaka 2020, asilimia 29 ya idadi ya watu wa Iran waliishi kwa mapato ya chini ya dola 6.85 kwa siku. Kwa kuzingatia hayo, takwimu za Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa hali ya Iran katika mistari yote mitatu ya umaskini iliyoainishwa na shirika hilo la kimataifa imeimarika kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka miwili ya serikali ya 13. Mbali na hayo kutolewa huduma kama vile bima ya msingi, suhula za afya katika vituo vya serikali, matibabu ya bure, utoaji wa posho kwa mama wanaonyonyesha na kulisha bila malipo watoto walio chini ya umri wa miaka 5 kumekuwa na nafasi muhimu katika kupunguza umaskini nchini.

Matokeo yaliyotajwa katika ripoti ya Benki ya Dunia na ripoti nyingine kama hizo kuhusu kuimarika kwa hali ya uchumi wa nchi licha ya kuendelea kuwekewa vikwazo, kwa upande mmoja, ni matokeo ya mbinu mpya zinazotekelezwa na serikali katika uwanja wa sera za kigeni, mbinu ambazo zimekuwa na matokea kama vile ya kuhuishwa uhusiano wa Iran na nchi za eneo na jirani, kuachiliwa pesa za Jamhuri ya Kiislamu na Korea Kusini na kupewa uanachama rasmi katika jumuiya za kimataifa kama vile za Shanghai na BRICS na kurejeshwa nafasi na itibari ya Iran katika shirika la mauzo ya mafuta la OPEC.

Wakati huo huo ushirikiano mzuri uliopo kati ya serikali na bunge umewezesha kupitishwa sheria muhimu kama vile Sheria ya Benki Kuu na mpango wa kodi ya biashara. Pia, muswada wa kodi ya mapato umekamilika na kuwasilishwa bungeni. Kwa kuzingatia hatua hizi za kimsingi, tunaweza kusema kwamba pamoja na kuwa kifo cha Ayatollah Raisi ni tukio chungu sana kwa taifa la Iran, lakini ni wazi kuwa hatua zilizochukuliwa na serikali yake zinaendelea kupunguza umaskini na kuimarisha uchumi nchini.