May 30, 2024 07:08 UTC
  • Kiongozi Muadhamu awaambia wanachuo US: Mpo katika upande sahihi wa historia

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria mwamko wa wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Marekani dhidi ya utawala katili wa Israel na kusisitiza kuwa, wanachuo hao wa US wamesimama katika upande sahihi wa historia.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema hayo katika barua yake ya wazi kwa wanachuo hao wa Marekani na kueleza kuwa, wanafunzi hao kwa kuwatetea wananchi madhulumu wa Palestina, sasa wamekuwa sehemu ya kambi ya muqawama ulimwenguni.

Katika barua hiyo, Kiongozi Muadhamu amewahutubu wanachuo wa Marekani kwa kusema; Hivi sasa mnaunda sehemu ya mrengo wa muqawama, na mumeanzisha mapambano ya heshima licha ya mashinikizo na mbinyo wa serikali yenu ambayo imekuwa ikiulinda utawala bandia na katili wa Kizayuni.

Ayatullah Khamenei ameeleza bayana kuwa, lengo la mapambano hayo ni kutaka kukomeshwa dhulma za wazi, ambazo mtandao wa kigaidi na kikatili wa 'Wazayuni' unawafanyia Wapalestina kwa miongo kadhaa sasa.

"Dhulma hizi zimepelekea Wazayuni wapore nchi ya Wapalestina, na kisha kuwaweka Wapalestina chini ya mashinikizo na ukandamizaji wa kutisha," ameongeza Kiongozi Muadhamu katika barua yake hiyo.

Kiongozi Muadhamu

Maandamano ya wanafunzi wanaounga mkono Palestina na kulaani jinai za utawala ghasibu wa Israel yaliyoanzia hivi karibuni katika Chuo Kikuu cha Columbia mjini New York, Marekani, yameenea katika vyuo vikuu vingine vya nchi hiyo na maeneo mengine ya dunia, licha ya kuendelea ukandamizaji wa viongozi na idara za nchi hiyo dhidi ya wanachuo. 

Moja ya sababu kuu za kuibuka vuguvugu la maandamano ya wanafunzi, ni jinai za kivita zinazotekelezwa na utawala haramu wa Israel dhidi ya watu wasio na hatia huko Gaza na ushiriki wa Marekani katika mauaji ya halaiki katika ukanda huo, na vile vile msaada wake mkubwa wa kifedha na silaha kwa utawala huo wa kibaguzi.

Ayatullah Ali Khamenei amesema, Palestina ni ardhi huru na taifa lenye Waislamu, Wakristo na Mayahudi, na pia ni taifa lenye historia ndefu, lakini baada ya Vita vya Pili vya Dunia, mabepari wa mtandao wa Kizayuni, kwa msaada na uungaji mkono wa serikali ya Uingereza, walianza kuingiza maelfu kadhaa ya magaidi katika ardhi hiyo.

Ameendelea kueleza kuwa: Walivamia miji na vijiji, ambapo makumi ya maelfu ya watu ama waliuawa au kuhamishiwa katika nchi nyingine, na kisha wakanyakua nyumba, masoko na mashamba yao, na baada ya hapo wakaunda serikali iliyopewa jina la Israel katika ardhi iliyoghusubiwa ya Wapalestina. 

Wanachuo Texas, US wakiandamana kuitetea Palestina licha ya mbinyo wa polisi

Ayatullah Khamenei ameongeza kwa kusema; Hatima nyingine inalisubiri eneo nyeti la Asia Magharibi, na dhamiri nyingi za watu zimeamka katika kiwango cha kimataifa, na ukweli unaendelea kufichuka. Kambi ya muqawama itapata nguvu zaidi, na historia pia inabadilika.

Barua hiyo ya Kiongozi Mkuu wa Iran kwa wanachuo wa Marekani imenukuu aya kadhaa za Qur'ani Tukufu ikiwemo aya ya 279 ya Sura al-Baqara (2) inayosema: Usidhulumu wala usidhulumiwe.

"Wasia wangu kwenu ni kwamba mjifunze Qur'ani Tukufu" imemalizia barua ya Kiongozi Muadhamu kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Marekani wanaondamana kuitetea Palestina.

Tags