Jun 17, 2024 02:55 UTC
  • Kaimu Rais wa Iran awapongeza Waislamu kwa mnasaba wa Idul Adh'ha

Kaimu Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyatumia ujumbe mataifa ya Kiislamu akiyapongeza kwa mnasaba wa kuadhimisha sikukuu ya Idul Adh'ha.

Katika jumbe tofauti aliowatumia marais na viongozi wa nchi za Kiislamu, Mohammad Mokhber amesema kuwa, anatumai tukio hili la kidini litaandaa mazingira ya kuhitimishwa mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. 

Mokhber amesema Idul Hajj ya mwaka huu inaadhimishwa katika hali ambayo, umma wa Kiislamu unawajihiwa na changamoto kubwa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, lakini nchi za Magharibi hazichukui hatua zozote za maana wakati ambapo wananchi wasio na hatia wa Palestina wanaendelea kuchinjwa na utawala wa Kizayuni.

Katika salamu zake hizo, Rais wa muda wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewapa mkono wa Idi viongozi wa nchi za Kiislamu na kueleza kwamba, sikukuu hii ni msimu wa kuuvua moyo na matashi kwa ajili ya Mola Mpendwa na kudhihirika imani na utiifu halisi mbele ya Muabudiwa.

Halikadhalika katika ujumbe wake huo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewaombea uzima na mafanikio viongozi; na saada na izza wananchi wa mataifa ya Kiislamu.

Idul Adh'ha, yaani sikukuu ya kuchinja au Idul-Hajj ni miongoni mwa sikukuu kubwa za Waislamu. Katika siku hii tukufu, Mahujaji waliokwenda kuzuru Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu huchinja kwa amri ya Mola na kwa ajili ya kupata radhi zake; na kwa kufanya hivyo, huendeleza na kuenzi kumbukumbu ya Mtume mteule wa Allah, Nabii Ibrahim (AS).

Baadhi ya nchi kama vile Saudi Arabia, Misri, Jordan, Palestina, Umoja wa Falme za Kiarabu, Tunisia, Algeria, na Libya zilitangaza jana Jumapili ya Julai 16 kuwa siku ya Idul al-Adh'ha.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Indonesia, Malaysia, Brunei, India na Oman pamoja na nchi kadhaa za Afrika zikiwemo Morocco na Mauritania zimetangaza kuwa, kwa kutegemea mwandamo wa mwezi, Jumatatu ya leo Juni 17 ndiyo sikukuu ya Idul Adh'ha.

Tags