Jun 17, 2024 07:46 UTC
  • Mokhber: Nchi za Waislamu ziungane kuzima jinai za Israel Gaza

Kaimu Rais wa Iran ametaka kuwepo umoja na mshikamano miongoni mwa nchi za Waislamu ili kukomesha jinai na mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Mohammad Mokhber ametoa mwito huo katika mazungumzo yake ya simu na Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif na kusisitiza kwamba, mataifa ya Kiislamu yanapaswa kutumia kila suhula yalizonazo ili kusitisha jinai za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza.

Mokhber amelipongeza taifa la Pakistan kwa kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina, na vile vile misimamo iliyo wazi ya serikali ya Islamabad ya kupinga jinai za Wazayuni katika eneo lililozingirwa la Gaza.

Amesisitizia haja ya nchi za Kiislamu kuchukua hatua ya kivitendo kwa ajili ya kukomesha jinai za Wazayuni huko katika Ukanda wa Gaza na pia katika maeneo mengine ya Wapalestina yanayokaliwa kwa mabavu.

Kadhalika Kaimu Rais wa Iran amekosoa undumakuwili wa Magharibi na kueleza kwamba, haingii akilini Wamagharibi kuwapa Wazayuni silaha na zana za kijeshi kwa upande mmoja, na wakati huo huo kudai eti inataka kushikamana na mpango wa kisiasa wa utatuzi wa mgogoro huo.

Rais wa muda wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameutaja mshikamano, umoja na mfungamano wa Waislamu kuwa ni jambo muhimu na la kistratijia, na njia pekee ya kukabiliana na njama za maadui.

Aidha ameashiria makubaliano yaliyosainiwa kati ya Tehran na Islamabad wakati wa ziara ya Shahidi Rais Ebrahim Raisi wa Iran huko nchini Pakistan. "Nchi mbili hizi zimekubaliana kuongeza ujazo wa biashara na mabadilishano ya kiuchumi hadi kufikia dola bilioni 10 kwa mwaka, tunatumai lengo hili muhimu litafikiwa kupitia juhudi za nchi mbili kuondoa vizingiti vya kibiashara," ameongeza Mokhber.

Tags