Gharibabadi: Marekani si mkweli kwa wananchi wa Iran
-
Kazem Gharibabadi
Katibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Iran amesema kuwa, Marekani si mkweli kwa wananchi wa Iran.
Kazem Gharibabadi amesema hayo katika mkutano na waandishi habari wa kupitia na kufichua haki za binadamu za Marekani na kueleza kwamba, jinai zilizofanywa na Marekani dhidi ya wananchi wa Iran hazipaswi kusahaulika.
Afisa huyo mwandamizi wa haki za binadamu nchini Iran amebainisha kwamba, wananchi na wanasiasa wanapaswa kuelewa kwamba, Marekani si mkweli kwa wananchi wa Iran.
Gharibabadi amesema bayana kwamba, hatua ya Marekani ya kuunga mkono makundi ya kigaidi hasa yaliyotenda jinai hapa nchini na wakati huo huo kuendelea kuliwekea vikwazo taifa la Iran ni ushahidi wa wazi kwamba, inasema uongo inapodai kwamba, inawaunga mkono wananchi wa Iran.
Katibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Iran amesema pia kuwa, vitendo visivyo vya kibinadamu na ukatili dhidi ya wanafunzi na maprofesa huko Marekani ni matukio ambayo yamewafunua macho walimwengu, na jinai ambazo Marekani imetenda dhidi ya watu wa Iran zinaonyesha mifano midogo ya muamala na utendaji wa Marekani ulio dhidi ya haki za binadamu.
Gharibabadi ameashiria matukio ya historia na kueleza kwamba, katika kipindi chote cha historia Marekani imefanya mauaji ya mamilioni ya watu wasio na hatia kama ambavyo imekiuka haki za wanawake na watu wa jamii za walio wachache nchini humo.