Jul 01, 2024 12:40 UTC
  • Iran yasema Hizbullah iko 'tayari kikamilifu' kukabiliana na vitisho vya Israel

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali Bagheri Kani, ameuonya utawala wa Israel kuhusu "matokeo mabaya" iwapo utaishambulia Lebanon, akisema harakati ya muqawama ya Lebanon, Hizbullah iko tayari kikamilifu kupambana na Israel.

Bagheri Kani ametoa onyo hilo katika mazungumzo yake ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, leo Jumatatu huku kukiwa na vitisho vya Israel vya kuanzisha mashambulizi dhidi ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon.

"Utawala wa Kizayuni wa Israel unapaswa kujua kwamba kosa lolote jipya utakalofanya nchini Lebanon litaibua mazingira mapya katika ngazi ya kieneo kwa hasara ya Wazayuni, ambao hawataweza kufidia kushindwa kwao kimkakati kwa kufanya mauaji na uhalifu," amesema mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran.

Bagheri Kani ameongeza kuwa, vitisho vya vita vya Israel dhidi ya Lebanon vinawiana na kuendelea jinai za utawala huo dhidi ya watu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza na vinaonyesha tabia yake ya kishenzi.

Kani ameashiria uwezo wa kipekee wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon ambayo imejitayarisha kikamilifu kukabiliana na vitisho vya utawala ghasibu wa Israel, na kuonya kwamba kitendo chochote cha uchokozi kitakuwa na gharama kubwa kwa wavamizi.

Kani: Hizbullah iko tayari kupambana na utawala katili wa Israel

Hali ya mvutano bado inashuhudiwa katika mpaka wa kusini wa Lebanon, ambapo Hizbullah inakabiliana na wanajeshi wa Israel ikilipiza kisasi cha mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo katili huko Palestina hususan katika Ukanda wa Gaza.