Jul 11, 2024 02:54 UTC
  • Dakta Masoud Pezeshkian
    Dakta Masoud Pezeshkian

Rais mteule wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian anatazamiwa kula kiapo cha kulitumikia taifa Julai 30 mwaka huu.

Hayo yalitangazwa jana Jumatano na Mojtaba Yousefi, mwanachama wa Bodi Andalizi ya Sherehe za Kumuapisha Rais ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran).

Mbunge huyo ameliambia shirika la habari la IRNA kuwa, mbali na maafisa wakuu wa Iran, viongozi kutoka mataifa mbalimbali duniani pia wanatazamiwa kuhudhuria hafla hiyo ya kuapishwa Rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu.

Yousefi ameeleza bayana kuwa, sherehe hiyo ya kumuapisha Masoud Pezeshkian itafanyika baada ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei kumuidhinisha rasmi rais huyo mpya wa Iran.

Dakta Pezeshkian mwenye umri wa miaka 69, alichaguliwa kuwa Rais wa tisa wa Iran baada ya kuibuka na ushindi wa kura milioni 16 na 384,403 kati ya zaidi ya kura milioni 30 zilizopigwa katika duru ya pili ya uchaguzi wa 14 wa Rais wa Iran Ijumaa iliyopita ya Julai 5. Mpinzani wake Saeed Jalili alipata kura 13,538,179.  

Rais mteule wa Iran, Masoud Pezeshkian anachukua usukani kuongoza serikali ya awamu ya 14 ya Iran, kufuatia kufa shahidi Rais Ebrahim Raisi katika ajali ya helikopta iliyotokea katika mkoa wa Azerbaijan Mashariki, mnamo Mei 19.

Tags