Jul 11, 2024 06:52 UTC
  • Idadi ya watu duniani yapindukia bilioni 8 huku idadi ya wanaozeeka ikiongezeka

Idadi ya watu duniani wenye umri wa miaka 65 na zaidi imeongezeka karibu mara mbili huku hali hii ikitazamiwa kuendelea. Idadi ya watu duniai inazidi kuongezeka katika pembe mbalimbali na tayari imepindukia watu bilioni 8.

Taarifa ya mwaka huu ya UN Population Fund (UNFPA) inaonyesha kuwepo mabadiliko makubwa katika mifumo ya ukuaji wa kikanda, msongamano wa watu, na viwango vya ukuaji wa miji. Kadiri idadi ya watu inavyoongezeka ulimwenguni kote; bara Ulaya, Amerika Kaskazini na maeneo ya Asia pia yanashuhudia ongezeko la idadi ya wazee, na hivyo kusababisha changamoto kwa huduma za afya, mipango ya kustaafu, na mifumo ya kazi.

Idadiya wazee inaongezeka Asia, Amerika ya Kaskazini na Ulaya 

Tarehe 11 Julai kila mwaka huadhimishwa kama "Siku ya Kimataifa ya Idadi ya Watu" lengo likiwa ni kuongeza uelewa wa masuala yanayohusiana na idadi ya watu duniani. Tarehe hii ilipewa jina hili baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1989 kukubali pendekezo la Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP). 

Afrika limetajwa kuwa bara linalokua kwa kasi huku ongezeko kubwa la watu likitarajiwa katika nchi za Nigeria, Ethiopia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na viwango vya juu vya uzazi na kuboreshwa kwa huduma za afya.

Ongezeko la idadi ya watu bado liko juu mashariki na kusini mwa Afrika huku kukiwa na jumla ya watu milioni 688, na Afrika Magharibi na Kati ikiwa na watu milioni 516.

Barani Asia nchi kama India na China zimekuwa na ongezeko la taratibu la idadi ya watu kutokana na kupungua kwa uzazi, huku mataifa ya Kusini-mashariki mwa Asia kama vile Indonesia na Ufilipino yakidumisha ukuaji wa wastani.

Tags