Mahakama Iran: Sharti US iwape fidia wagonjwa wa kipepeo kutokana na vikwazo
Mahakama moja nchini Iran imeiagiza Marekani kulipa takriban dola bilioni 7 kama fidia kwa waathiriwa wa ugonjwa wa ngozi wa Epidermolysis Bullosa (EB) nchini Iran.
Katika uamuzi wake wa jana Alkhamisi, Mahakama ya Haki ya Mahusiano ya Kimataifa (Tawi la 55) mjini Tehran ilisema serikali ya Marekani inatakiwa kulipa fidia ya dola bilioni 6.78 kwa wagonjwa wa kipepeo (EB) Wairani, ambao hali zao zimezidi kuwa mbaya kutokana na vikwazo vya Washington kwa sekta ya afya ya Iran.
Mahakama hiyo imesema vikwazo hivyo vya Marekai vimezuia wagonjwa hao kufikia baadhi ya haki zao za kibinadamu zikiwemo za kujidhaminia usalama wa maisha na afya. Imefafanua kuwa, taathira hasi za vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran zimepeleka waathirika wa magonjwa sugu na maalumu kama vile wagonjwa wa kipepeo wakabiliwe na matatizo makubwa katika kujidhaminia dawa za kupunguza makali ya maradhi hayo.
Katika miaka michache iliyopita, makumi ya watoto waliokuwa wakisumbuliwa na maradhi ya kipepeo walipoteza maisha kutokana na ukosefu wa dawa na vifaa tiba vya kudhibiti maradhi hayo hapa nchini.
Athari mbaya za vikwazo vya nchi za Magharibi hasa Marekani dhidi ya Iran haziwaathiri wagonjwa wa ngozi ya kipepeo peke yao, bali hata wagonjwa wa thalassemia na watu wengine wenye magonjwa maalumu pia wako katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na vikwazo hivyo.
Si vibaya kuashiria hapa kuwa, kampuni moja ya Sweden ilikataa kutuma bandeji za matibabu kwa wagonjwa wa ngozi ya kipepeo (EB) nchini Iran kutokana na vikwazo vya Marekani. Karibu wagonjwa 1,200 wa ugonjwa wa ngozi wa kipepeo nchini Iran wanahitaji haraka bandeji hizo za matibabu.